2013-07-16 09:52:23

Padre William Nordenbrock, C.PP.S. achaguliwa kuwa Mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu duniani: 2013 - 2019


Wajumbe wa mkutano mkuu wa 20 wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu wamemchagua Mheshimiwa Padre William Nordenbrock kutoka Kanda ya Cincinnati, Marekani, kuwa Mkuu mpya wa Shirika. Padre Nordenbrock anachukua nafasi ya Mheshimiwa Padre Francis Bartoloni, aliyemaliza muda wake.

Takwimu za Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi zinaonesha kwamba, hadi kufikia Mwezi Mei 2013, kulikuwa na jumla ya Wanashirika 562, wanaoishi na kutekeleza utume wao katika nchi 22. Barani Afrika Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu wanafanya kazi nchini Tanzania na Guinea Bissau. Mkutano mkuu wa 20 umefafanua dira itakayoongoza Shirika kuanzia mwaka 2013 hadi mwaka 2019.

Katika Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika kwenye Kikanisa cha Makao Makuu ya Kanda ya Italia, mjini Roma na kuongozwa na Mheshimiwa Padre William Nordenbrock, aliwaalika kwa namna ya pekee Wamissionari wa damu Azizi ya Yesu, kujichotea huruma kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwani hiki ni kiini cha upendo unaojenga na kudumisha mshikamano wa dhati kati yao na Mwenyezi Mungu.

Amemshukuru Padre Francis Bartoloni aliyempatia fursa ya kujifunza mengi kutoka kwake kama Mkuu wa Shirika Msaidizi. Ni matumaini yake kwamba, hazina na utajiri aliojichotea utamsaidia kutekeleza dira na mwelekeo wa Shirika katika kipindi cha miaka sita ijayo.

Katika mahubiri yake Mheshimiwa Padre Francis Bartoloni amewashukuru wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirika kwa kazi nzuri walioifanya, huku wakionesha moyo wa upendo na mshikamano wa dhati. Katika kipindi chote cha uongozi wa ngazi ya juu Shirikani, amejifunza kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu, Kanisa na Shirika katika ujumla wake; ameonja upendo na uvumilivu kutoka kwa Wanashirika wenzake, lakini bado kuna changamoto kubwa ya kuendelea kujifunza mahangaiko ya watu, ili kujibu kilio cha damu kwa watu wa nyakati hizi.

Anawataka Wamissionari kumwilisha changamoto inayoendelea kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko ya kutoka waliko, ili kuwaendelea wale ambao wamesukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana na uwepo wa dhambi, athari za utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Ni mwaliko wa kuwa kweli ni vyombo vya upatanisho unaolenga kuleta mageuzi ulimwenguni na katika Kanisa. Tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu, iwe ni dira itakayowawezesha kutekeleza dhamana hii kwanza kabisa kwa kujikita katika maisha ya Sala, Tafakari ya Neno la Mungu pamoja na kusikilizana.

Padre Francis Bartoloni ambaye kabla ya kuchaguliwa kwake kuwa Makamu mkuu wa Shirika na baadaye kuwa mkuu wa Shirika, aliishi na kufanya utume wake nchini Tanzania katika Majimbo ya Singida, Dodoma, Morogoro na hatimaye Jimbo kuu la Dar es Salaam amsema, kwa sasa yuko tayari kupokea utume mwingine kadiri ya mapenzi ya wakuu wake wa Shirika.

Mara baada ya mahubiri, Padre Francis alimkabidhi Padre William Nordenbrock mshumaa wa Shirika, tayari kuwaingiza Wanashirika katika awamu nyingine ya uongozi huku wakitembea katika Mwanga wa Kristo Mfufuka. Padre Bill kama anavyoitwa na wengi, alikiri Kanuni ya Imani na baadaye Ibada ya Misa Takatifu ikaendelea kama kawaida.







All the contents on this site are copyrighted ©.