Wanajeshi 7 wa Tanzania wauwawa na wengine 14 wajeruhiwa Darfur, Sudan
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi,
Jakaya Mrisho Kikwete ameshtushwa na kuhuzunishwa sana na tukio la kushambuliwa na
kuuawa kwa vijana saba hodari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania waliokuwa wanalinda
amani katika eneo la Darfur, Sudan.
Kwa hakika, Rais amesikitishwa sana na
kitendo hicho ambako wanajeshi wengine 14 wa Tanzania wamejeruhiwa na waasi wa Sudan
na ametuma salamu za rambirambi za moyoni mwake kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania
na kwa familia za wafiwa wote.
Aidha, Rais Kikwete anaungana na Watanzania
wote na hasa maofisa na wapiganaji wa JWTZ na familia za wafiwa kuomboleza vifo vya
vijana hao hodari wa Tanzania. Rais pia anaungana na Watanzania wote kuwaombea wale
walioumia katika tukio hilo waweze kupona haraka na kuendelea na majukumu yao ya ulinzi
wa amani chini ya Umoja wa Mataifa.
Katika salamu zake za rambirambi kwa Mkuu
wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Adolf Mwamunynge na familia za wafiwa, Rais Kikwete
na Amiri Jeshi Mkuu amesema: “Sina maneno ya kutosha ya kuelezea mshtuko, huzuni na
masikitiko yangu makubwa kufuatia vifo vya vijana wetu hao ambao wamepoteza maisha
yao katika shughuli muhimu sana ya utekelezaji wa majukumu ya Umoja wa Mataifa ya
kulinda na kuleta amani katika eneo la dunia ambako maelfu kwa maelfu ya watu wamepoteza
maisha yao kwa kushambuliwa na waassi.”
Rais Kikwete ameongeza kumwambia Mkuu
wa Majeshi ya Ulinzi na familia za wafiwa ”Napenda kwa niaba ya Watanzania wenzangu
niwahakikishieni kwamba hakuna shaka kuwa vijana wetu hao tokea walipokwenda Darfur
Februari mwaka huu, na kwa hakika tokea Tanzania ilipoanza kuchangia walinzi katika
eneo hilo mwaka 2007, wamefanya kazi nzuri sana, kazi iliyoongozwa na weledi wa hali
ya juu na kazi ambayo imeiletea nchi yetu heshima kubwa. Tutaendelea kuwaenzi kwa
kujivunia kazi yao.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Nakutumia wewe Mkuu wa Majeshi
ya Ulinzi salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza vijana wetu hawa.
Kupitia kwao, natuma salamu za rambirambi kwa maofisa wakuu na maofisa wadogo pamoja
na wapigaji wote wa Jeshi letu kwa kupotelewa na wenzao. “
“Aidha, kupitia
kwako, natuma salamu zangu kwa wanafamilia za waliopotelewa na wapenzi wao na ndugu
zao katika tukio hilo. Wajulishe kuwa naungana nao katika kuomboleza. Wajue kuwa uchungu
wao ni uchungu wangu pia na wa Watanzania wote na kuwa kwa pamoja tunamwomba Mwenyezi
Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu. Vile vile kwa
pamoja tunamwomba Mwenyezi Mungu azilaze peponi roho za marehemu. Amina”.
Kwa
walioumia, Rais Kikwete amemwambia Jenerali Mwamunyange: “Naungana pia na Watanzania
wenzangu katika kuwapa pole nyingi walioumia katika tukio hilo tukiwaombea kwa Mwenyezi
Mungu wapone haraka na kuendelea na shughuli zao za ulinzi wa amani chini ya Umoja
wa Mataifa.”
Vijana hao waliopoteza maisha yao na walioumia, walikuwa sehemu
ya askari 37 na ofisa mmoja ambao walikuwa wanasindikiza msafara wa waangalizi wa
kijeshi katika Darfur kutoka eneo la Khorabeche kwenda Nyara waliposhambuliwa na waasi
kiasi cha kilomita 20 kutoka Khor Abeche saa tatuna nusu asubuhi, Jumamosi, Julai
13, 2013.