2013-07-15 10:50:35

Jumuiya ya Kimataifa yalaani mauaji ya Askari wa kulinda amani, Darfur, Sudan


Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon amesikitishwa na kuhuzunishwa na mauaji ya wanajeshi saba kutoka Tanzania waliokuwa wanalinda amani, Darfur, Sudan baada ya kushambuliwa na Waasi wa Sudan. Katika tukio hilo, wanajeshi wengine kumi na wanne walijeruhiwa. Tukio hili limelaaniwa pia na viongozi mbali mbali wa Jumuiya ya Kimataifa.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anaitaka Serikali ya Sudan kuhakikisha kwamba, inawatafuta wahusika na kuwafikisha mbele ya mkondo wa sheria ili kujibu tuhuma za mauaji. Hili ni tukio la tatu katika kipindi cha majuma matatu yaliyopita.

Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania anaungana na watanzania wengine kuomboleza vifo vya askari hawa na kwamba, Wanajeshi wa Tanzania wataendelea kutekeleza dhamana na majukumu yao ya ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa huko Sudan, ambako hali bado ni tete. Wanajeshi waliouwawa ni sehemu ya kikosi cha wanajeshi 37 waliokuwa wanaelekea Nyala, waliposhambulia na waasi wa Sudan, kiasi cha kilomita 20 hivi kutoka Khor Abeche, Kusini mwa Sudan, Jumamosi, majira ya saa 3:30 asubuhi.

Wanadiplomasia wanasema kwamba, jumla ya wanajeshi 16,000 walioko kwenye Vikosi vya Kulinda Amani vya Umoja wa Mataifa wanakabiliana na uhaba wa vifaa vya kijeshi, mafunzo hafifu na baadhi ya Serikali za Kiafrika kutoonesha ushirikiano wa kutosha kwa kupeleka wanajeshi katika maeneo ambayo yanasadikiwa kuwa tete! Zaidi ya Askari 50 kutoka katika vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa nchini Sudan, UNAMID wamekwisha poteza maisha tangu mwaka 2007.







All the contents on this site are copyrighted ©.