Hata wavuvi wanasubiri kusikia Habari Njema ya Wokovu!
Chukua nyavu zako tweka hadi kilindini, ndiyo kauli mbiu inayoongoza Maadhimisho ya
Siku kuu ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli, Msimamizi wa Mabaharia inayoadhimishwa
na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 16 Julai.
Baraza la
Maaskofu Katoliki Hispania katika Maadhimishi haya sanjari na Mwaka wa Imani, wanawaalika
waamini kwa namna ya pekee, kuhakikisha kwamba, Yesu kristo anakuwa ni kiini cha maisha
na shughuli zao za kila siku na kwa njia hii, wanaweza kupokea changamoto kutoka kwa
Kristo anayewataka kutweka hadi kilindini licha ya kazi kubwa waliyoifanya usiku kucha
lakini wakaambulia patupu!
Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania, linapenda
kuwashirikisha Mabaharia ile furaha ya imani kwa Kristo na Kanisa lake, kama sehemu
ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya, dhamana ambayo inavaliwa njuga na Mama Kanisa katika
Mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema
wanaalikwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa
kwa sura na mfano wa Mungu.
Inasikitisha kuona kwamba, Mabaharia wengi wananyanyaswa
na kudhulumiwa na kwamba, utu na heshima yao wakati mwingine havipewi kipaumbele cha
kwanza, bali watu wanaangalia zaidi faida inayozalishwa na Mabaharia hawa, hata kama
inawagharimu maisha na utu wao! Hapa Waswahili wangeweza kusema, “Punda afe lakini
mzigo ufike”.
Maaskofu wanabainisha kwamba, utume wa Bahari unaotekelezwa na
Mama Kanisa kwa miaka mingi sasa unapania kwa namna ya pekee kabisa kuwasaidia waamini
katika hija ya maisha yao ya Imani kwa Kristo na Kanisa lake. Ni utume unaolenga kuwasaidia
Mabaharia kukabiliana na fursa, changamoto na matatizo wanayokumbana nayo kila siku
wanapotekeleza wajibu wao.
Kwa njia ya ushuhuda wa upendo na mshikamano, Kanisa
pia linapenda kuwahimiza waamini kuzisaidia familia za Mabaharia ambazo mara nyingi
zinakabiliwa na hali ngumu ya maisha. Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linakumbuka
changamoto zilizotolewa na Washiriki wa Kongamano la ya 23 la Utume wa Bahari lililofanyika
mjini Roma, Mwezi Novemba, 2012, kwa kukazia utume wa Kanisa katika kuwahudumia Mabaharia
na mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, wahusika wanaendelea kuboresha
hali ya maisha ya Mabaharia pamoja na vitendea kazi vyao.
Mwishoni, Maaskofu
wa Hispania wanasema, wanapenda kumwilisha katika vipaumbele vyao vya shughuli za
kichungaji, changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko ya kutoka katika ubinafsi
wao na kuanza kujimwaga pembezoni mwa Jamii kwa ajili ya kuwainjilisha wale wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii ili nao pia waweze kuonja ile furaha ya kuwa ni wafuasi wa Yesu.
Kwa tukio hili, waamini wanachangamotishwa kwenda kwenye fukwe za bahari ili
kuwainjilisha hata Mabaharia kwa njia ya ushuhuda wa maisha amini na matakatifu. Mabaharia
wanaonesha moyo wa matumaini ya kutaka kukutana na Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na
kufufuka kutoka katika wafu; Kristo anayetangazwa na kushuhudiwa na Mama Kanisa katika
maisha na utume wake, hasa miongoni mwa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.