2013-07-13 09:39:48

Vijana kutoka Senegal waanza safari kuelekea Rio de Janeiro! Kumekucha!


Ujumbe wa vijana ishirini kutoka Majimbo Katoliki Senegal, umepokea bendera ya taifa lao, tayari kuanza hija ya kwenda kwenye Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2013 inayoanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 23 hadi tarehe 28 Julai 2013.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukamilisha maandalizi ya mwisho, kabla ya "kutinga timu" nchini Brazil. Vijana waliochaguliwa ni wale ambao wameonesha mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa, Majimboni mwao, kiasi kwamba, wamechaguliwa na Maaskofu mahalia, ili waweze kuwa kweli ni chumvi na mwanga kwa vijana wenzao nchini Senegal. Serikali ya Senegela imechangia sehemu ya gharama kwa vijana hawa ili kuwawezesha kuungana na vijana wenzao kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Serikali ya Senegal inasema, majiundo makini kwa vijana ni muhimu sana katika mchakato wa kukuza na kuimarisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kitamaduni pamoja na mshikamano miongoni mwa watu wa kimataifa. Wawakilishi wa Senegal wametakiwa kuonesha mfano bora wa kuigwa na vijana wenzao wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Wawe ni mahujaji wanaowajibika na kuheshimu sheria na kanuni za nchi.

Taarifa zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya waandishi wa vyombo mbali mbali vya habari wapatao 5, 500 waliojiandikisha kutoa taarifa wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Brazil. Waandishi 2,000 ni wale wanaotoka kwenye vyombo vya habari kimataifa. Idadi ya waandishi habari inatazamiwa kuvuka ya wale waliohusika na kurusha habari katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2011 iliyofanyika Jimbo kuu la Madrid, Hispania.







All the contents on this site are copyrighted ©.