Upendo na huruma vinavyomwilishwa katika huduma: kiroho na kimwili
Shirika la Masista wa Upendo la Huruma wa Mtakatifu Vincent wa Paulo, Mitundu, Singida,
Tanzania linalojiandaa kuwa ni Kanda kamili panapo majaliwa mwishoni mwa Mwaka 2013,
hivi karibuni, limemwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuwajalia
kupata watawa wapya tisa, kati yao nane walifunga nadhiri za kwanza na mtawa mmoja
alifunga nadhiri zake za daima.
Ibada ya Misa
Takatifu iliyoongozwa na Mheshimiwa Padre Francis Lyimu, msaidizi wa Askofu msimamizi
wa kitume wa Jimbo Katoliki Singida na kupokelewa na Sr. Verediana Herman, Mama Mkuu
wa Kanda. Hadi sasa Shirika la Masista wa Upendo la Huruma wa Mtakatifu Vincent wa
Paulo, Mitundu linatekeleza dhamana na wajibu wake wa kichungaji katika Majimbo ya
Singida, Mbeya, Kigoma na Jimbo kuu la Dar es Salaam.
Wamejikita katika utoaji
wa huduma ya afya, elimu na maendeleo endelevu yanayotafsiriwa kwa namna ya pekee
katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Masista hawa wanaongozwa na fadhila
za Mtakatifu Vincent wa Paulo, yaani kuwahudumia na kuwainjilisha maskini. Masista
hawa wanaongozwa na roho ya shirika inayowasukuma kuonesha moyo wa unyenyekevu, unyofu,
upendo na huruma.
Utume huu unajielekeza zaidi katika kumfuasa Kristo aliyejitoa
bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwatangazia maskini Habari Njema ya Wokovu; kuishi
na kumwilsiha kanuni ya maisha; kuonesha upendo na ibada kwa mwenyezi Mungu kwa njia
ya huruma kwa maskini pamoja na kuishi fadhila zinazoongoza maisha na utume wao: unyenyekevu,
unyofu, upole, kujitiisha kwa hiyari kwa ajili ya wokovu wa watu.