2013-07-13 08:40:20

Siku ya utume wa bahari, tarehe 14 Julai 2013


Mama Kanisa kila mwaka ifikapo Jumapili ya Pili ya Mwezi Julai, anaadhimisha Siku ya Utume wa Bahari. Hiki ni kipindi cha sala, tafakari na shukrani kwa Mabaharia wanaotolea maisha yao kwa ajili ya huduma kwa Jumuiya ya Kimataifa. Takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 90 ya mizigo yote duniani inasafirishwa kwa njia ya bahari.

Maadhimisho haya pia yanalenga kuwatia shime Walezi wa kiroho na watu wanaojitolea kusonga mbele kwa imani na matumaini. Itakumbukwa kwamba, Utume wa Bahari ulianzishwa kunako mwaka 1920. Sekta ya usafiri baharini inakumbana na changamoto nyingi hasa wakati huu wa utandawazi. Jambo la kusikitisha aliwahi kusema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, ni kuona kwamba, nyanyaso na madhulumu kwa Mabaharia yanazidi kuongezeka. Ni kundi ambalo linakabiliwa na utekaji nyara unaofanywa na maharamia baharini, kutelekezwa na waajiri wao kwa kipindi kirefu sanjari na athari za uvuvi haramu unaotishia maisha ya viumbe hai baharini.

Hayo yamo kwenye ujumbe uliotolewa na Kardinali Antonio Maria VegliĆ², Rais wa Baraza la Kipapa la wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi, katika Maadhimisho ya Siku ya Utume wa Bahari kwa Mwaka 2013. Kongamano la Utume wa Bahari lililofanyika mjini Vatican kunako mwaka 2012 kwa kuwashirikisha wajumbe 260 kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ni kielelezo makini kwamba, Mama Kanisa anapenda kutoa huduma ya kiroho na kimwili kwa mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao.

Hii ni changamoto kwa Wakristo na wadau mbali mbali kutambua mchango unaotolewa na Mabaharia sehemu mbali mbali za dunia na changamoto wanazokumbana nazo! Mkataba wa Mwaka 2006 uliotolewa na Shirika la Kazi Duniani utaanza kutumika rasmi mwezi Agosti 2013 baada ya kuridhiwa na nchi wanachama 30 wa Shirika la Kazi Duniani. Utekelezaji huu ni matokeo ya majadiliano na upembuzi yakinifu ulionza kujitokeza kunako mwaka 1920. Mkataba huu unabainisha haki msingi za mabaharia, hali yao ya maisha, maeneo ya kazi, usawa, huduma, hifadhi za kijamii pamoja na haki ya kutembelea miundo mbali mbali wanapotua nanga bandarini ili kupata tiba na huduma muhimu.

Baraza la Kipapa linaunga mkono mktaba huu kwa kutoa fursa kwa Mabaharia kuweza kupata huduma ya afya na ustawi wa maisha yao wanapokuwa bandarini. Nchi wanachama zinapaswa kutekeleza dhamana hii kwa kuzingatia misingi ya haki, usawa, ukweli na uwazi. Mamlaka za Bandari zisaidie kuhakikisha kwamba, zinatenga fungu litakalowahudumia Mabaharia wanapokutana na matatizo kazini.

Mikataba ya kimataifa iliyowekwa tangu mwaka 1973 hadi mwaka 2006 ina umuhimu wa pekee katika kudhibiti uchafuzi wa mazingira, huduma kwa Mabaharia, viwango na ubora wa kimataifa. Mabaharia wanapaswa kujibidisha kuifahamu mikataba hii kwa ajili ya mafao yao binafasi na ustawi wa huduma za mabaharia kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Kardinali Antonio Maria VegliĆ² anawaombea wadau mbali mbali wa utume wa Bahari ili waweze kusindikizwa katika maisha na utume wao na Bikira Maria nyota ya bahari.







All the contents on this site are copyrighted ©.