2013-07-13 13:48:30

Mwaka wa Imani na maisha ya mchanganyiko kijamii


Makala Dunia Mama, yanaendelea kuchambua maisha katika mtazamo wa mwaka wa imani, tukizama zaidi katika maisha hali halisi za mchanganyiko wa tamaduni mbalimbali.
Tunapozungumzia mada hii ni muhimu kwanza kujua sababu zinazofanya watu leo hii wachanganyike sana kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma ambako watu waliishi kimakundi makundi katika misingi ya kifamilia, ukoo au ukabila, wakibaki katika eneo moja, kizazi hadi kizazi.
Kwa kusoma matukio ya kihistoria ya maisha ya kijamii, tunaona kuna mabadiliko makubwa kwa nyakati hizi. Nyakati hizi watu wanapenda kwenda huko na kule bila kujali kuwa mbali na jamaa zao. Na kwa nini inakuwa hivyo? Kuna sababu nyingi zinazoleta hali hiyo. Kwanza ni ufahamu kwamba, binadamu wote ni sawa, wote wameumbwa kwa sura moja na mfano wa Mungu, hivyo uwepo wa mtu mahali popote, unapata heshima yake, tofauti na zamani, ambapo mtu mgeni, mara nyingi alionekana kama adui anayeingilia eneo la wengine.
Heshima na uhuru huu wa binadamu ,unaimarishwa na azimio la Umoja wa Mataifa la haki za binadamu, lililopitishwa na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa Desemba 10, 1948, kama matokeo ya vita kuu ya pili ya dunia. Azimio hili la Dunia, lenye kutoa msisitizo kwamba, maisha ya kila binadamu yanapaswa kuheshimiwa. Na hivyo ni azimio hilo huimarisha ustaraabu wa kuheshimiana na maisha ya binadamu kulindwa kama kitu cha thamani.
Kwa azimio hilo, msingi wa ustaraabu kuthamini na kuyaheshimu maisha ya binadamu, inakuwa ni haki yenye thamani kubwa machoni pa wengine. Na pia , inakuwa ni kichochea kikubwa cha watu kupenda kuhama toka sehemu moja hadi nyingi, hasa pale hali za maisha zinapokuwa ngumu, iwe ni kutokana na machafuko ya kisiasa au ugumu wa uchumi. Walau mkimbizi au mhamiaji anajua kwamba ni haki yake kuyasalimisha maisha yake dhidi ya maoenevu yanayomsonga.
Pia leo hii, jambo hili la kuhamahama linarahisishwa zaidi na kuboreka kwa teknolojia hasa za njia za usafiri na mawasiliano. Mtu hahitaji tena kutembea kwa masiku au miezi kutoka sehemu moja au nyingine. Nyakati za ujima mtu wa Afrika Kusini kwenda Kenya ilikuwa ni ndoto ya kufikirika isiyowezekana.Lakini leo hii ni safari ya nusu siku. Maendeleo haya kwa kadri ya mapito ya nyakati, yamefanya utendaji wa binadamu, kuwa na mpanuko mkubwa zaidi kifikira na kitendaji. , Aidha kwa njia ya elimu, binadamu wa siku hizi, amewezeshwa kufahamu haki zake msingi kama binadamu , haki ya kuishi, haki ya kuwa na makazi , haki ya kupata chakula na maji na huduma za afya na maendeleo yake kwa ujumla.
Katika uchambuzi wa haki hizo , kila binadamu anapata ufahamu kwamba anayo haki ya kuishi, mahali popote katika dunia hii, na hivyo hupata nguvu na kishawishi cha kwenda kutafuta mahali anapoweza kuinua hali ya maisha yake. Maana dunia iliumbwa na Mwenyezi Mungu na kuvikabidhi vyote vilivyomo katika usimamizi wa binadamu. Hivyo mipaka ya nchi iliyopo ni mipaka iliyowekwa na binadamu na si Mungu.
Kwa muono huo, Mababa wa Kanisa katika Mkutano wao Mkuu wa Pili wa Vatican, walioona kwamba, ni wajibu wa kudumu wa kanisa, kuchunguza ishara za nyakati na kuzifafanua katika mwanga wa Injili, ili kwamba kwa namna hiyo, na katika kila kizazi , kanisa liweze kuyajibu masuala yanayojirudia mara kwa mara , mintarafu katika maana ya maisha ya kisasa na ya wakati ujao hasa mahusiano ya kila siku ya binadamu.
Kanisa linatambua , binadamu leo hii anaishi katika kipindi kipya cha historia yake , kipindi chenye kuwa na mvuto wa mabadiliko ya haraka yenye kuenea kwa kasi kama moto uwakao katika nyasi kavu ulimwenguni. Kasi hii inashamirishwa na kasi ya maendeleo ya ufahamu na teknolojia, ikimwezesha mtu kuyaona haraka yanayompendeza na kumvutia na hivyo matamanio ya toka sehemu moja hadi nyingine kwa muda mfupi, huurarua moyo wa mtu, katika matamanio ya kutaka kuingia katika maisha mapya yanayomvutia.
Askofu Mkuu Agostino Marchetto, Katibu katika Sekretariat ya Baraza la Kipapa kwa ajili ya kazi za Kichungaji kwa Wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, akitoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Diego cha Marekani , aliitaja tabia ya uhamiaji kuwa ni ishara ya nyakati zetu , ni ishara yenye kuwa na shauku za utendaji mpya , unao zua wimbi la watu kuhamia huko na kule.
Ni wazi wimbi hili, kwa baadhi ya serikali na taasisi , huliona ni jambo la hatari na hivyo hujenga hofu, mashaka na wasiwazi kwa wageni , na hivyo hutafuta namna za kudhibiti, ikiwezekana hata kukomesha. Lakini , katika ustaraabu wa leo hii, kama ilivyoelezwa hapo juu, binadamu wa leo si kama wa zamani. Leo hii , binadamu ameelimika na ana ufahamu zaidi wa haki zake kama binadamu , na kwa msaada wa teknolojia ya mawasialiano na usafiri inakuwa si jambo jepesi kuzuia watu wasihame toka eneo moja hadi jingine.
Hotuba ya Askofu Mkuu Marchetto, iliendelea kusema, ni wazi, Wahamiaji huondoka katika nchi yao ya kuzaliwa na kuvuka mipaka ya nchi nyingine, wakiwa na utambulisho na sifa zao na kukutana na watu wengine waliokulia mazingira tofauti , waliopokea elimu na majiundo tofauti , pengine hata huzumgumza lugha tofauti na kula milo tofauti. Tofauti hizi zinaweza kuleta usumbufu fulani au kukosesha raha hasa wenyeji ambao ni wengi kuliko kundi la wahamiaji.
Kanisa linasema, tofauti hizo , hazipaswi kuwa sababu msingi ya kumnyanyapaa mgeni mhamiaji au mkimbizi , kwa sababu tofauti hizo ni mazoea ya kijamii, ambayo hayaondoi heshima ya utu wa mtu alioumbwa nao na Mwenyezi Mungu. Na ndiyo maana Kanisa Katoliki, husisitiza haja ya kuwandaa watu kwa ajili ya uhamiaji, kupitia mipango ya elimu , malezi na mafundisho, ili kwa wanaolenga kuhama waweza kuendana na hali watakazo zikuta mahali wanapotaka kuhamia na pia kwa ajili ya kuwapokea wageni wanaoingia katika sehemu zao kama ilivyoelezwa katika sheria na Kanuni za kichungaji( Art 18. 1).

Na kama alivyoeleza Papa Yohane Paulo 11 wakati akiuhutubia mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa Octoba 5, 1995 kwamba, “Mhamiaji anapoingia katika mazingira mapya , utendaji wake , unaweza kuwa wa nguvu katika kuibua upya ufahamu wa tabia zake, kimila na kitamaduni, kama haja ya kutaka kudumisha utambulisho wake kimaisha”. Hupata mwamko wa kujitambua zaidi yeye ni nani, hasa pale anapo kosa kuwaona watu walio muhimu zaidi kwake , kama wazazi, wake au waume, watoto na jamaa zake. Na hivyo huwa na mwelekeo wa kutafuta faraja na usalama wake kwa wale wanatoka taifa moja, au wenye kuwa na utamaduni unaofanana. Na polepole hutafuta kuendeleza mfumo wa maisha waliozoea makwao . Wakati huohuo, wenyeji , nao huwa na mashaka na wageni na mara nyingi hukataa kuwapokea kama walivyo , kwa hofu za kuhatarisha mila , utamaduni na utambulisho wa jamii mahalia. Hivyo mitazamo hii, huongoza katika uundaji a magenge magenge kulingana na mahali mtu alikotoka na utambulisho wake, na huo unakuwa mwanzo wa kubaguana na kunyanyasana.
Hotuba ya Papa yohane Paulo 11 , kwa ajili ya Siku ya Dunia ya Wahamiaji 2005, ili angalisha kwa namna gani inawezekana kutengeneza mahusiano mazuri kati ya wahamiaji na wenyeji wao , akishauri kwamba, njia inayo faa na ya ukweli, ni njia ya umoja na ushirikiano wa kweli thabiti. Ushirikiano ulio wazi, mmoja akijifunua kwa mwingine, kukaribisha na kuwapokea wageni kwa jinsi walivyo na utamaduni wao, katika hali za kuheshimiana na kujaliana , na hivyo sura ya jamii na tamaduni inapata kuwa sura ya nyuso mbalimbali kama zawadi ya Mungu kwa binadamu. Na hivyo tofauti za utambulisho wa kiutamaduni, unapata kufunua ulimwengu mpya wa maelewao yasiyo fungamana na upande mmoja, lakini wenye kuwa na mtazamo chanya katika huduma ya familia yote ya binadamu.

Ni wazi , ushirikiano huu ni safari ndefu tena ya polepole , lakini ni mchakato pekee unaofaa, si tu kama wajibu wa wahamiaji lakini pia wenyeji , kutembea katika njia hii ambayo mna uwezekano wa kugundua siri za maisha ya mmoja kwa mwingine, kupitia maisha ya pamoja. Pande zote mbili, ni lazima kuwa tayari kupitia utaratibu huu, mazungumzano yakiwa ni “injini” ya ushirikiano huo. Ushirikiano wa kweli hufanyika kwa uwepo wa mwingiliano mzuri baina ya wahamiaji na wenyeji, si tu kijamii na kiuchumi, lakini pia katika ngazi ya utamaduni wenye kuwa na kiasi, na ujenzi wa mazingira ya kirafiki na mshikamano tulivu.
Kule kutambua mchango chanya wa wahamiaji kwa wenyeji, utamaduni wao na vipaji vya wahamiaji, inakuwa ni motisha ya ujenzi wa mwingiliano zaidi kwa wenyeji. Na hivyo inakuwa ni sababu chanya ya kuwa na ushirikiano imara zaidi.
Aidha Yohane Paulo II, alitaja haja ya mazungumzo kati ya watu wa tamaduni mbalimbali, kwamba ni suala linaloenda zaidi ya kuvumiliana, na kuwa suala la huruma na huduma.
Nyenzo ya Mazungumzo hulinda utambulisho dhahiri wa tamaduni na pia ni silaha yenye kudumisha maelewano na umoja kwa pande zote. Kama matokeo yake, hutajirisha tamaduni na jamii kuheshimiana, na jamii kubadilika katika mpangilio wake wa maisha, ikiruhusu, kila utamaduni kupata nafasi yake na kuunda kitu kimoja lakini chenye kuwa na rangi mbalimbali za utamaduni, ukitoa picha ya kupendeza zaidi katika msururu wa ongezeko tamaduni, kulingana na mpango huo wa umoja katika jamii ya binadamu wote.
Imeandaliwa na T.J.Mhella.







All the contents on this site are copyrighted ©.