2013-07-13 11:18:58

Migomo ya kila siku inafisha tija na ufanisi shuleni!


Watoto ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa; walelewe vyema na kurithishwa tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu. Wapewe elimu itakayowasaidia kupambana na changamoto za maisha, wakiwa makini katika imani, maadili na utu wema.

Ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Askofu msaidizi David Kamau wa Jimbo kuu la Nairobi, wakati alipokuwa anaadhimisha Ibada ya Misa takatifu katika shule ya "Mary Queen" iliyoko Jijini Nairobi, inayomilikiwa na kuendeshwa na Shirika la Waconsolata wanaofanya utume wao nchini Kenya. Shule hii ambayo inatoa elimu ya msingi na sekondari ilianzishwa kunako mwaka 2004. Ina jumla ya wanafunzi 300 na walimu 40.

Askofu Kamau anasema, ndama ni muhimu sana katika zizi, kwani bila Ndama, zizi linaweza kukauka, ndivyo ilivyo pia kwa Familia, kwani Familia bila watoto waliolelewa vyema ni sawa na gari lisilokuwa na mafuta, haliwezi kutembea! Wazazi wanapaswa kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika Jamii na kuonesha mafao ya elimu waliyoipata.

Haitoshi kwenda shule tu, bali mtu anapaswa kuelimika na kwamba, elimu yake imsaidie kupambana na changamoto za maisha. Elimu ya kwanza inajikita katika uchaji wa Mungu, pale mwanadamu anapompatia Mungu heshima na nafasi yake. Walimu watambue haki na wajibu katika kurithisha ufahamu kwa wanafunzi waliokabidhiwa kwao.

Migomo ya mara kwa mara inayofanywa na walimu nchini Kenya inaweza kushusha kiwango cha elimu kama hatua madhubuti hazitaweza kuchukuliwa mapema iwezekanavyo. Majadiliano kati ya Serikali na Walimu ni jambo la msingi ili kudumisha tija na ufanisi katika sekta ya elimu. Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Kenya linawapongeza Wamissionari wa Consolata katika utume wao katika sekta ya elimu.







All the contents on this site are copyrighted ©.