2013-07-13 10:55:10

Kuna uhusiano wa pekee kati ya: shule, familia na parokia


Kanisa Katoliki Barani Afrika limekuwa ni mdau mkubwa katika utoaji wa huduma kwenye sekta ya elimu kuanzia kwenye ngazi ya elimu ya awali hadi elimu ya juu. Katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina, Kanisa nchini Mauritius linapenda kujikita katika sehemu kuu tatu yaani: Familia, Shule na Parokia. Huu ni mkakati wa Uinjilishaji wa kina unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2013 hadi mwaka 2016.

Mwaka wa kwanza, Kanisa litajikita zaidi kwa kukazia majiundo makini shuleni, kwa kuwekeza zaidi na zaidi, ili elimu inayotolewa na Kanisa Katoliki nchini humo iendelee kukidhi viwango na mahitaji ya wananchi wa Mauritius; kwa kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuihudumia nchi yao kwa moyo na ari kubwa zaidi. Ustawi na maendeleo ya nchi yanapata chimbuko lake katika msingi bora wa elimu. Kanisa Katoliki nchini Mauritius linatambua na kuthamini mchango unaotolewa na Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume katika sekta ya elimu.

Shule na taasisi za elimu zinapaswa kuwa ni madaraja yanayojenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa, kwa kutambua na kuthamini tofauti za kidini, kiimani na kitamaduni, lakini mambo yote haya yawe ni sehemu ya utajiri wa wananchi wa Mauritius na kamwe yasiwe ni kizingiti wa kikwazo cha kuwagawa watu. Maadili na utu wema na mambo msingi katika sekta ya elimu, vinginevyo vijana wanaweza kujikuta wanaelemewa mno na malimwengu kiasi cha kushindwa kutambua na kuenzi tunu msingi za maisha na maadili ya Kiafrika kutokana na athari za utandawazi.

Hii ndiyo mikakati ya shughuli za kichungaji iliyopembuliwa hivi karibuni na Askofu Maurice Piat wa Jimbo la Port-Louis, nchini Mauritius. Kanisa linapenda kuangalia kwa namna ya pekee dhamana na utume wake katika sekta ya elimu, kwa kukazia utofauti unaojisimika katika umoja na mshikamano, kwani kuna uhusiano mkubwa kati ya: Elimu, Parokia na Familia kama inavyobainishwa kwenye "Mradi wa Kleopas".

Kanisa linapenda kujikita zaidi pia katika kuimarisha Katekesi, ili waamini waweze kufahamu kuhusu Mafundisho tanzu ya Kanisa na wawe tayari kuyatolea ushuhuda katika maisha na vipaumbele vyao. Jamii ijifunze kujenga na kuimarisha majadiliano ya kidini na kiimani, yanayofumbatwa katika msingi wa ukweli na uwazi pamoja na kuthaminiana. Waamini katika mchakato kama huu, watambue Imani ya Kanisa Katoliki pamoja na kuendelea kuwanoa Makatekista, ili waweze kutekeleza utume wao kikamilifu katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi ya ajabu.

Vyama vya kitume na familia katika Parokia ni muhimu sana katika kujenga na kuimarisha utambulisho na mshikamano wa Familia ya Mungu inayowajibika. Waamini washirikishe karama, vipaji na taaluma zao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu katika ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa. Kila mwamini anakumbushwa kutekeleza dhamana na wajibu wake kama Mbatizwa na raia mwema.







All the contents on this site are copyrighted ©.