2013-07-12 14:32:40

Yaliyojiri kwenye Mkutano wa 16 wa SECAM huko DRC


Wajumbe wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM katika mkutano wao wa kumi na sita, wameendelea kujadili kwa kina na mapana changamoto zilizotolewa na Mababa wa Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika kuhusu: haki, amani na upatanisho.

Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kinshasa, DRC, amekazia umuhimu wa ukweli na upatanisho mintarafu mwanga wa Waraka wa Dhamana ya Afrika uliotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, kama njia ya kuponya madonda ya chuki, uhasama na utengano miongoni mwa Jamii nyingi za Kiafrika.

Wajumbe wamezungumzia kuhusu umuhimu wa tume za haki na amani za Mabaraza ya Maaskofu Katoliki katika kukuza na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene kama sehemu ya Uinjilishaji wa kina Barani Afrika, ili kujenga na kuimarisha Jamii zinazosimikwa katika misingi ya haki,amani, upendo na mshikamano wa kweli.

Wajumbe wamekazia pia Utume wa Biblia Barani Afrika. Wameipembua SECAM kwa kuonesha nguvu na udhaifu wake katika kutekeleza maamuzi pamoja na kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika.

Wajumbe wa SECAM, siku ya Ijumaa wamekutana na kuzungumza na Rais Joseph Kabila wa DRC. Jumatano jioni, wajumbe wa SECAM walikaribishwa kwenye Ubalozi wa Vatican nchini DRC kwa tafrija fupi. Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa SECAM amemshukuru Askofu mkuu Tito YIlana kwa moyo wa ukarimu na upendo kwa wajumbe wa SECAM.







All the contents on this site are copyrighted ©.