2013-07-11 11:57:29

Tafsiri ya Rasimu ya Katiba Mpya Tanzania kwa Umombo ina mapungufu!


Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa ufafanuzi kuhusu Rasimu ya Katiba iliyotolewa hivi karibuni katika lugha Kiingereza na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na kusema rasimu hiyo haitoi tafsiri sahihi ya maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyozinduliwa na Makamu wa Rais, Dkt. Mohammed Gharib Bilal Juni 3, 2013.

Rasimu hiyo iliyotolewa na LHRC ambayo inasambazwa kupitia njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii, pia inatumika katika mikutano na warsha mbalimbali zinazojadili kwa lengo la kutoa maoni kuhusu Rasimu iliyotolewa na Tume.

“Tume ya Mabadiliko ya Katiba inapenda kuwafahamisha wananchi na wadau wengine kuwa Rasimu hiyo ya Katiba katika lugha ya kiingereza iliyoandaliwa na LHRC haitoi tafsiri sahihi ya maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume katika lugha ya Kiswahili na hivyo kupotosha umma kuhusu maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyotolewa hivi karibuni,” amesema Katibu wa Tume hiyo, Bw. Assaa Rashid katika taarifa yake kwa Vyombo vya Habari Julai 9, 2013.

Bw. Asaa amewataka wananchi kuendelea kusoma na kutoa maoni kuhusu Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika lugha ya Kiswahili ambayo amesema imesambazwa kwa wananchi, taasisi, jumuiya na taasisi mbalimbali. Rasimu hiyo pia inapatikana katika tovuti ya Tume () na kutolewa bure katika Ofisi za Tume zilizopo Dar es Salaam na Zanzibar.

Aidha, Tume hiyo imesema iliandaa Rasimu ya Katiba katika lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha wananchi ambao wengi wao wanajua kusoma na kuandika kwa lugha ya Kiswahili kuelewa maudhui ya Rasimu hiyo.

Katika taarifa yake, Tume imewataka wadau wote wanaotaka kutafsiri Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume kuwasiliana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ina Wataalamu wa Uandishi wa Sheria (Legislative Drafters).








All the contents on this site are copyrighted ©.