Baraza la Maaskofu katoliki Hispania hivi karibuni limehitimisha mkutano wake wa mia
mbili na ishirini na nane, uliojadili pamoja na mambo mengine, taarifa ya Tume ya
Elimu na Katekesi ya Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania katika mkakati wa maboresho
ya elimu.
Maaskofu
wamepembua pia taarifa ya Jumuiya ya Kimataifa kuhusu afya n avigezo vya elimu ya
uzazi salama. Huu ni mwongozo uliotolewa kwa ajili ya wadau wanaojihusisha na uundaji
wa sera za elimu na masuala ya afya.
Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania
limeonesha wasi wasi wake kutokana na mapungufu makubwa yaliyojitokeza kwenye mwongozo
huu, unaopaswa kutumiwa na nchi za Ulaya. Vigezo vilivyotolewa, havigusii hata kidogo
kanuni maadili na utu wema, mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa na wadau wa elimu
na afya, katika mchakato wa kumhudumia mtu mzima.
Baraza la Maaskofu kwa kuguswa
na changamoto hizi, limeamua kuanza kuandaa hati ambayo itaihusisha Jumuiya ya Kikristo
mintarafu kweli za kweli za Kiinjili, tunu msingi za maisha na wito wa ndoa na familia,
kama sehemu ya majiundo ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Baraza la Maaskofu
limepitia pia kanuni msingi zinazopaswa kutekelezwa na taasisi za Kanisa katika huduma
ya elimu na afya. Kanuni hizi zitafanyiwa kazi katika mkutano wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Hispania, kwenye mkutano wao ujao. Wanaangalia pia jinsi ya kukabiliana na
changamoto za kimaadili na utu wema katika masuala ya elimu na afya kwa kuunda Tume
moja ya Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania itakayokuwa na wajibu wa kutoa ushauri
katika masuala nyeti ya elimu, afya na jamii. Wanaangalia pia uwezekano wa kuunda
Tume ya Uinjilishaji Mpya na Katekesi.