2013-07-11 07:56:50

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani: Kumekucha!


Padre Andrea Koprowski, Mkurugenzi wa vipindi Radio Vatican anapenda kuwaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kuanza kuyaelekeza macho na mawazo yao kwenye Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani itakayoanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 23 hadi tarehe 28 Julai 2013 huko mjini Rio de Janeiro, Brazil. Wachunguzi wa mambo wanasema, Maadhimisho ya Mwaka huu, kwa hakika utakuwa ni moto wa kuotea mbali, mwenye macho haambiwi tazama! RealAudioMP3

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwamba, wanabeba ndani mwao chemchemi ya furaha ya imani na kwamba, hawana sababu yoyote ya kuuonea aibu Msalaba wa Kristo, badala yake wawe na ujasiri wa kuukumbatia kwani wanatambua kwamba, hii ni zawadi ya pekee kutoka kwa Kristo na chemchemi ya furaha ya kweli kwani kwa njia ya Fumbo la Msalaba Yesu ameweza kushinda dhambi na mauti.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwaalika vijana kubeba Msalaba na kuendelea kuutembeza katika hija ya maisha yao sehemu mbali mbali za dunia. Hivi ndivyo Baba Mtakatifu Francisko alivyowakumbusha vijana wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kijimbo ambayo hufanyika kila mwaka wakati wa Jumapili ya Matawi. Kwa mwaka huu, Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ulifurika kwa umati wa vijana kutoka kila pembe ya dunia.

Anasema, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ni kiini cha matumaini ya Kikristo. Huu ndio ukweli wanaopaswa kuubeba na kuwashirikisha wengine, wakitambua kwamba, Yesu anaendelea kutembea pamoja nao hata katika maisha ya ujana wao. Huu ndio utume wa vijana, mashahidi wa Kristo, wanaopaswa kumshuhudia Kristo kwa njia ya maisha yao adili, kwa kutambua kwamba, Kristo ni mzima na Yeye ndiye chemchemi ya matumaini ya kweli katika ulimwengu huu ambayo umeathirika kutokana na vita, migogoro, kinzani, ubaya na dhambi.

Ni jukumu na dhamana ya vijana kuhakikisha kwamba, wanatolea ushuhuda wa matumaini mapya. Ndivyo Baba Mtakatifu Francisko alivyowachangamotisha vijana wakati wa Katekesi yake mwanzo mwa mwezi Aprili, 2013. Padre Koprowski anasema, mahubiri ya Baba Mtakatifu Francisko yameanza kuonesha dira na mwelekeo katika hija ya Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani itakayofanyika huko Rio de Janeiro. Hili ni tukio lenye kubeba mapana katika Maadhimisho yake, kwa kuonesha kwamba, Kanisa ambalo ni fumbo la Mwili wa Kristo linaendelea kufanya hija kutoka katika kizazi kimoja hadi kingine.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2013 yatakuwa na mambo mengi mapya, kwani kwa mara ya pili, Maadhimisho haya yanafanyika Amerika ya Kusini na kwa namna ya pekee nchini Brazil. Hii ni nchi ambayo imekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha na kuimarisha dhamana ya Kanisa katika shughuli na utume wa Kimissionari Amerika ya Kusini. Idadi kubwa ya vijana wataoshiriki ni wale wanaotoka katika nchi jirani, sehemu ambako imani inaadhimishwa kwa kuonesha ile furaha ya maisha ya Kijumuiya, haya ni matunda ya kazi kubwa iliyofanywa na Familia ya Mungu Amerika ya Kusini katika dhamana ya Uinjilishaji, changamoto iliyotolewa kwa namna ya pekee na Mkutano wa Maaskofu wa Amerika ya Kusini uliofanyika kule Aparecida. Hii ni furaha ya kweli inayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo.

Padre Koprowiski anabainisha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko kwa hakika atakuwa ni kivutio cha pekee katika maadhimisho haya, kwa kutambua kwamba, Yeye anatoka katika nchi jirani ya Argentina, lakini kwa sasa anawakilisha Kanisa la Kiulimwengu akiwa na mwono mpana zaidi.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake ameendelea kuonesha umuhimu wa Fumbo la Msalaba katika maisha na utume wa Kanisa. Msalaba ni fumbo linalogusa uhalisia wa maisha ya watu. Akiwa Askofu mkuu Kardinali Bergoglio aligusa na kuguswa na matatizo ya wananchi wa Argentina na Amerika ya Kusini katika ujumla wake.

Ameshiriki na kuchangia kwa kina na mapana katika Maadhimisho ya Mikutano ya Uinjilishaji Amerika ya Kusini. Ni Kiongozi anayetarajiwa kuzungumzia kiini cha matatizo ya watu wa Amerika ya Kusini na hatimaye, kuwaonesha vijana dira na mwelekeo katika kupambana na changamoto hizi zote kwa imani na matumaini kwa Kristo na Kanisa lake. Vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia watakuwa na mchango wao maalum katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013.

Itakumbukwa kwamba, Amerika ya Kusini ina namna yake ya pekee kabisa katika maadhimisho ya Imani. Lakini, wachunguzi wa mambo wanasema, furaha ni kati ya zawadi kubwa ambayo wale wote watakaojitaabisha kuhudhuria Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Rio de Janeiro wataonja.

Wataonja ukarimu wa wenyeji wa Maadhimisho haya kwani kuna jumla ya vijana elfu kumi watakaotoa huduma ya kujitolea kwa vijana zaidi ya millioni mbili kutoka katika kila pembe ya dunia. Haya yote ni matunda ya Imani na mwaliko wa Mama Kanisa kuendelea kufanya majadiliano ya kina na wale wasioamini, lakini wanayo hamu ya kutaka kumfahamu Mwenyezi Mungu.

Kardinali Bergoglio katika barua yake ya kichungaji kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, alipembua kwa kina na mapana dhana ya “Mlango” mintarafu hali na mazingira ya nyakati hizi.

Kutokana na ukosefu wa usalama, amani na utulivu, watu wengi wamejikuta wanafunga milango ya nyumba na maisha yao kwa wageni na watu wasiowafahamu, ili kujihakikishia usalama wa maisha. Mlango uliofungwa ni kielelezo makini cha maisha ya Jamii nyingi katika ulimwengu mamboleo, ni hali halisi inayoyojionesha kwa sasa na kwa siku za usoni katika kukabiliana na changamoto za maisha.

Mlango uliofungwa madhubuti ni kielelezo pia cha mtu kujifunga katika undani wa maisha yake, zile ndoto, matumaini, mahangaiko na nyakati za furaha zinafungwa na hivyo kushindwa kuwashirikisha majirani na watu wengine. Mlango uliofungwa ni kielelezo cha moyo uliofungwa pia kwa watu wengine, kiasi kwamba watu wengi zaidi wanashindwa kupita na hatimaye, kushiriki undani wa maisha ya mtu. Kimsingi, mlango uliofunguliwa daima umekuwa ni kielelezo cha mwanga, urafiki, furaha, uhuru na uaminifu.

Padre Andrea Koprowski katika tafakari hii ya kina, anasema, Baba Mtakatifu Francisko anawachangamotisha waamini kutokatishwa tamaa na magumu wanayokabiliana nayo katika hija yao ya maisha, bali, kuwa na mwono na mwelekeo mpya wa maisha unaoboreshwa kwa njia ya haki na utakatifu wa maisha; kwa kuwaendea wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kwa kuwaita kwa majina yao halisi.

Kanisa linapaswa kufungua malango yake ili kuwapokea wale wote wanaomtafuta Kristo katika hija ya maisha yao, lakini pia linapaswa kutoka kifua mbele kwenda kutangaza Injili ya Kristo sehemu mbali mbali za dunia kwa watu wa nyakati hizi wanaokumbana na ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Itakumbukwa kwamba, Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni sherehe ya urafiki, imani, furaha na umoja. Baba Mtakatifu Francisko anakumbusha kwamba, Kanisa linatumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu, kwa kuwaondolea watu dhambi zao, ili kuwawezesha kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu; kwa kupanda mbegu ya haki na amani mioyoni mwa watu ili kuifanya dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Roho wa Kristo Mfufuka aliwawezesha Mitume wa Yesu waliokuwa wamejifungia ndani kwenye chumba cha juu kwa woga wa Wayahudi kutoka kifua mbele kutangaza Injili ya Kristo.

Waamini katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo wanayo dhamana ya kumshuhudia Kristo kwa ujasiri mkubwa pasi ya woga wowote. Wakristo wajitahidi kuishi ukristo wao kama wafuasi makini wa Kristo. Hii ndiyo changamoto kubwa inayowakabili Wakristo kwa sasa kutokana na mazingira na hali ngumu inayowakabili, lakini, wanapaswa kujenga na kuimarisha mazingira ya kuzima kiu ya watu katika ukweli; kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wawe tayari kulinda na kutunza mazingira ambayo ni sehemu ya kazi ya Uumbaji.

Mji wa Rio de Janeiro una hifadhi kubwa ya anuai ya kimataifa. Kunako mwaka 2012 ulikuwa ni mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa maendeleo endelelevu uliojulikana kama “Rio + 20”, yaani: Shirikisho la Nchi Ishirini zinazoendelea Duniani. Ni mkutano ambao uliweka mikakati ya ushirikiano baina ya Jumuiya ya Kimataifa: kwa nchi zilizoendelea na zile ambazo kwa sasa zinaibukia katika maendeleo.

Hizi ni nchi kama vile: Brazil, India, China na Afrika ya Kusini. Lengo ni kushirikiana ili kujenga na kuimarisha uchumi wa kijani unaosimikwa katika matumizi sahihi ya rasilimali ya dunia. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni kielelezo cha mshikamano wa kimataifa. Jumuiya ya Kimataifa inabainisha matumaini ya watu kwa siku za usoni, lakini haitoshi kuwa na nyaraka zilizoandikwa vyema lakini bila utekelezaji. Kuna haja pia ya kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya zinazoendelea kuleta athari kubwa katika maisha ya vijana.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, aliwahi kusema kwamba, Kanisa kwa siku za usoni litaibuka kutoka katika vyama vya kitume na makundi ya waamini ambao kwa pamoja wataweka amana ya imani yao katika ushuhuda halisi wa maisha. Hili litakuwa ni Kanisa ambalo litajikita zaidi katika maisha ya kiroho bila kuingilia sana masuala ya kisiasa.

Litakuwa ni Kanisa linaloelezea ufukara wa Kristo na hapo, Kanisa litakuwa na mvuto wa pekee kwani watu wengi wataweza kuona utofauti na upya wa maisha ya waamini kwa njia ya ushuhuda wao wenye mvuto na mashiko. Haya ndiyo matumaini ya Kanisa kwa siku za usoni. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni kielelezo makini cha maisha ya kiroho, ni changamoto kutoka kwa vijana wanaotafuta maana halisi ya maisha na matumaini yao!

Padre Andrea Koprowski anahitimisha tafakari yake ya kina kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa kuonesha mwendelezo makini wa ukuaji na ukomavu wa Kanisa katika utume wake kama sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo unaotoa maisha mapya kwa ulimwengu.

Imehaririwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.