Askofu mkuu Lebulu: haki, amani na upatanisho ni chanda na pete!
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa Kumi na sita, katika Waraka wake Dhamana ya Afrika
anabainisha kwamba, Kristo katika moyo wa maisha ya Kiafrika anapaswa kuwa ni chemchemi
ya upatanisho, haki na amani na kwamba, Kanisa lina mchango wa pekee kabisa Barani
Afrika katika kuhamasisha na kumwilisha tunu hizi msingi katika maendeleo na ustawi
wa Bara la Afrika.
Upatanisho
na haki ni mhimili mkuu wa amani ambayo kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi
Mungu. Hii ni amani inayobubujika katika haki, ukweli na upendo unaojenga na kuimarisha
kifungu cha upendo na udugu katika Familia ya Mungu inayowajibika. Haki inafumbatwa
katika fadhila ya ukweli.
Ni changamoto inayotolewa na Askofu Mkuu Josephat
Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania. Anasema, amani inagusa undani na moyo wa
mtu. Ni fadhila inayogusa mahusiano, upendo, ukweli na unyofu wa moyo. Amani inajikita
katika kulinda na kutunza mazingira, ambayo ni sehemu ya kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi
Mungu amemkabidhi mwanadamu kuyatunza na kuyaendeleza kwa ajili ya mafao ya sasa na
kwa ajili ya kizazi kijacho.
Askofu mkuu Lebulu anasema kwamba, amani ni fadhila
inayodai uwajibikaji wa kiuchumi, kijamii na kisiasa. Kukosa na kukoseana ni sehemu
ya ubinadamu, kupatana na kusahau ni mwanzo wa hija ya maisha ya utakatifu na maendeleo
endelevu, changamoto kwa watu kujenga ndani mwao utamaduni wa msamaha na upatanisho,
kama kielelezo cha amani ya kweli!