Ukarimu ni sehemu ya tunu msingi za maisha ya kiroho!
Hija ya Kichungaji iliyofanywa na Baba Mtakatifu Francisko, Kisiwani Lampedusa, Kusini
mwa Italia, Jumatatu, tarehe 8 Julai 2013 ni changamoto kwa viongozi wa kidini kutambua
adha na mahangaiko ya mamillioni ya wakimbizi kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaotafuta
usalama wa maisha.
Ni watu wanaopaswa kuonjeshwa upendo na ukarimu; kwa kuheshimu
na kuthamini utu wao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Watu wajenge
utamaduni wa ukarimu kwa kuwapokea wakimbizi na wahamiaji kama ndugu zao! Lakini kwa
bahati mbaya, licha ya mateso na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji hawa kutoka
sehemu mbali mbali za dunia, wanapofika Barani Ulaya, wanabaguliwa na kunyanyaswa,
hali ambayo inaongeza machungu katika maisha ya wakimbizi hawa.
Taarifa zinaonesha
kwamba, kuna zaidi ya wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum wapatao
millioni arobaini, waliotawanyika sehemu mbali mbali za dunia.
Ni maneno ya
Kardinali Rodrigues Maradiaga, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa
Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, wakati huu Jumuiya ya Kimataifa inapoendelea
kufanya tafakari ya kina kama sehemu ya kuamsha dhamiri, ili hatimaye, kutambua na
kuchukua hatua madhubuti ili kushughulikia tatizo la wakimbizi na wahamiaji wanaokufa
maji wakati wakiwa njiani kutafuta hifadhi ya maisha Barani Ulaya.
Kardinali
Maradiaga anasema, Mwezi Novemba mwaka huu, kutafanyika mkutano mkuu wa viongozi wa
kidini wapatao 400 ili kuzungumzia dhana ya ukarimu mintarafu dini mbali mbali duniani,
kwani kama viongozi wa kidini wanalo jukumu la kuwalinda na kuwakirimia wakimbizi,
wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Ukarimu ni sehemu ya mafundisho na tunu
msingi za maisha ya kiroho.