Rehema kutolewa wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013
Katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 yanayoongozwa na kauli
mbiu "Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa ni wanafunzi" kuanzia tarehe 22
hadi tarehe 29 Julai 2013, sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliotangazwa
na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, Papa Francisko
anapenda kuwaalika vijana na waamini katika ujumla wao, kujipatia rehema kamili na
rehema ya muda kwa kutimiza masharti yaliyowekwa na Mama Kanisa.
Rehema kamili
inaweza kupatikana mara moja kwa siku, ikiwa kama mwamini atatimiza mashari kwa kuungama,
kupokea Ekaristi Takatifu na kusali kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu Francisko pamoja
na kuwakumbuka marehemu waamini waliolala kwenye usingizi wa amani, wakiwa na tumaini
la ufufuko wa wafu. Waamini wanaalikwa kufanya toba na wongofu wa ndani, ili kuweza
kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013.
Kwa
waamini ambao hawaweza kuhudhuria katika Maadhimisho ya Vijana kihalali, wanaweza
pia kupata rehema kamili, ikiwa kama watatimiza masharti yaliwekwa na Mama Kanisa,
kwa kufuatilia matukio hayo kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya kijamii.
Kanisa
linatoa pia rehema ya muda kwa waamini wote watakaotimiza masharti yaliyotajwa, kwa
ajili ya kuombea mafanikio ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013,
wakiwa na moyo wa toba na ibada; kwa kusali kwa Bikira Maria, Mama yetu wa Brazil
pamoja na Watakatifu na wenyeheri wasimamizi wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.
Lengo ni kuombea uthabiti wa imani miongoni mwa vijana ili hatimaye, waweze
kutembelea katika utakatifu wa maisha. Mapadre waliotubu na wenye moyo wa ibada wanaweza
kutekeleza dhamana hii kwa ajili ya waamini wanaotaka kupata rehema kamili na rehema
ya muda wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.
Itakumbukwa
kwamba, rehema ni ondoleo mbele ya Mungu adhabu za muda iliyostahiliwa kutokana
na dhambi ambazo kosa lao lilikwishasamehewa. Kwa kutimiza masharti yaliyopangwa,
mwamini anapata ondoleo hilo kwa ajili yake au ya marehemu kwa huduma ya Kanisa ambalo,
kama msimamizi wa neema za ukombozi, anagawa hazina ya mastahili ya Kristo na ya Watakatifu.