Jamii za Kiafrika hazina budi kujipanga vyema ili kukabiliana na ongezeko la idadi
ya wazee watakaohitaji huduma makini za Kijamii!
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaikawa Bwana, Jumapili iliyopita
tarehe 7 Julai 2013, alitambua uwepo wa Wanajumuiya ya Mtakatifu Egidio, waliokuwa
wanahudhuria mkutano wa waratibu wa Jumuiya za Mtakatifu Egidio kutoka Afrika na Amerika
ya Kusini.
Mkutano huu
umehudhuriwa na Queen Said, Mratibu wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, Tanzania anayeelezea
kwa kina na mapana yaliyojiri kwenye mkutano huo. Anasema, wamejadili mbinu mkakati
wa kupambana na changamoto mbali mbali zinazoibuliwa katika ulimwengu wa utandawazi
na maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na kuangalia jinsi ya kupanua wigo wa
utume wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, ili iweze kuwafikia watu wengi zaidi.
Lengo
la Jumuiya hii ni kutaka kuwa ni sauti ya wanyonge na wote wanaosukumizwa pembezoni
mwa Jamii; watu ambao utu na heshima yao inabezwa na kutwezwa. Maendeleo ya sayansi
na tiba ya mwanadamu yamesaidia kuboresha hali ya maisha ya watu wengi duniani. Kwa
sasa umri wa kuishi umeongezeka maradufu, ikilinganishwa na miaka kadhaa iliyopita.
Hii ina maanisha kwamba, katika miaka michache ijayo, hata Bara la Afrika litakuwa
na idadi kubwa ya wazee, watakaohitaji huduma mbali mbali za kijamii.
Queen
Said anasema, umefika wakati kwa Jamii za Kiafrika kuanza kujipanga vyema, kwani kwa
miaka mingi hili halikuwa ni tatizo kutokana na idadi ya wazee kuwa ni wachache kiasi
kwamba, waliweza kuhudumiwa katika Familia na Koo zao. Mambo yana badilika kwa kasi,
wazee wengi wanaanza kuachwa peke kutokana na sababu mbali mbali.
Kumbe, kuna
haja ya kujipanga vyema, ili kuimarisha huduma kwa wazee kwa siku za usoni sanjari
na kuimarisha tunu msingi za maisha ya kifamilia, ili wazee hawa waweze kufurahia
uzee wao badala ya kutelekezwa kwenye nyumba za wazee au kuachwa wakitangaza tanga
barabarani ili kujipatia riziki yao kana kwamba, hawakuwa na ndugu wala Jamaa!
Jumuiya
ya Mtakatifu Egidio inaendelea kutoa huduma kwa wagonjwa wa Ukimwi kwa njia ya Mradi
wake maarufu unaojulikana kama "The Dream" unaotoa dawa za kurefusha maisha kwa wagonjwa
wa Ukimwi pamoja na kuhakikisha kwamba, wanapunguza maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi
kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto bila kusahau maboresho ya huduma ya lishe ili kujenga
mwili uweze kupambana vyema na magonjwa nyemelezi.
Mradi wa "The Dream" Uko
sehemu mbali mbali Barani Afrika na kwa namna ya pekee umeonesha mafanikio makubwa
nchini Malawi. Nchini Tanzania, mradi huu unatekelezwa USA-Riva na Mkoani Iringa.