2013-07-10 08:20:36

Idadi ya wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi inazidi kuongezeka maradufu!


Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, katika kikao cha hamsini na saba cha Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, alionesha wasi wasi wa ujumbe wa Vatican kwenye mkutano huu, kutokana na ongezeko la idadi ya wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi duniani katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. RealAudioMP3

Hii inatokana na ukweli kwamba, kumekuwepo na vita, kinzani na migogoro ya kijamii ambayo imepelekea watu wengi kuyakimbia makazi yao.

Hali hii inaonesha pia kwamba, kunakosekana utashi wa kisiasa unaoweza kusukuma majadiliano ya kina ili kupata suluhu ya kudumu katika migogoro hii ambayo inaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Wajumbe wa Vatican wanaendelea kukazia kwamba, kwa njia ya vita, mambo mengi yanapotea na kuharibika, lakini amani, inalinda na kutunza yaliyokwishafikiwa na Jamii husika, kumbe kuna haja ya kuwekeza katika kulinda na kutunza amani.

Askofu mkuu Tomasi, anampongeza Kamishina mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa kwa kuanza kushirikisha taasisi za kidini katika kuwahudumia wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi na kwamba, jitihada hizi zimeanza kuonesha mafanikio. Taasisi hizi zimekuwa ni chemchemi ya faraja, mshikamano na majadiliano yanayojengwa katika msingi wa kueshimiana na kuthaminiana kwa ajili ya mafao ya wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum.

Hizi ni Jumuiya ambazo kimsingi zinalenga kualinda wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum. Mashirika ya Misaada ya Kidini Kimataifa kwa sasa yanaendelea kutoa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria, mahali ambako mtutu wa bunduki unaendelea kutishia usalama na maisha ya watu wengi ndani na nje ya Syria yenyewe.

Mashirika hayo yanaendelea kutoa tiba, chakula, malazi na ushauri nasaha, kwa zaidi ya watu laki moja walioko kwenye maeneo ya Damasko, Homs, Aleppo na Vijiji vinavyozunguka miji hii. Huduma hii inatolewa bila ubaguzi wa aina yoyote ile, kwani kinachoangaliwa hapa ni mtu na wala si imani wala mahali anakotoka. Mashirika haya yanatekeleza huduma zake zinazoongozwa na kanuni ya mshikamano.

Askofu mkuu Tomasi anazipongeza nchi za Yordani, Lebanon, Uturuki na Iraq kwa kuendelea kupokea wakimbizi zaidi ya million moja kutoka Syria, jambo ambalo limekuwa ni changamoto kubwa kwa nchi zinazotoa hifadhi kwa watu hawa pamoja na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa. Lakini, kuna haja ya kuwa makini zaidi, kwani Jumuiya ya Kimataifa inapoelekeza macho yake ya huruma kwa wananchi wa Syria wanaokabiliana na hali ngumu ya maisha.

Kuna hatari kwamba, wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi sehemu nyingine za dunia wakaathirika, kutokana na ukosefu wa rasilimali fedha! Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kukumbuka kwamba, maisha ya binadamu yana thamani kubwa, yanapaswa kulindwa na kuheshimiwa. Watu wanaokimbia nchi zao ili kusalimisha maisha yao, wanapaswa kupewa hifadhi na nchi husika sanjari na kuhudumiwa na Jumuiya ya Kimataifa.

Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi anahitimisha kwa kusema kwamba, kuna haja ya kuwa sera na mikakati makini katika kuwahudumia wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi sehemu mbali mbali za dunia.








All the contents on this site are copyrighted ©.