Wakimbizi na wahamiaji waguswa na uwepo na maneno ya Papa Francisko Kisiwani Lampedusa!
Hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko Kisiwani Lampedusa imelenga kuamsha
tena dhamiri za watu ili waguswe na mateso pamoja na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji
wanaopoteza maisha yao baharini kwa kuwa na tumaini la maisha bora Barani Ulaya. Umefika
wakati wa kuondokana na utandawazi usiojali na kukumbatia utandawazi unaojikita katika
ukarimu na mshikamano wa upendo.
Baba Mtakatifu akiwa Kisiwani Lampedusa ametupa
shada la maua baharini kwa ajili ya wale waliopoteza maisha yao wakiwa njiani kuja
Barani Ulaya. Amepata fursa ya kuzungumza na wakimbizi pamoja na wahamiaji wengi wao
wakiwa ni wale wanaotoka Barani Afrika. Baba Mtakatifu aliwashukuru wahamiaji waliompokea
katika makazi yao na kuwahakikishia kwamba, lengo lake Kisiwani hapo lilikuwa ni kuwaombea
na wao pia kumwombea yeye katika maisha na utume wake.
Baba Mtakatifu amesali
hata kwa wale ambao kutokana na sababu mbali mbali hawakuweza kufika katika Ibada
ya Misa Takatifu iliyohudhuriwa na umati mkubwa wa watu. Wakimbizi wamemwambia Baba
Mtakatifu kwamba, wao wanatafuta hifadhi ya kisiasa kwani wamekimbia nchi zao kwa
sababu za kisiasa na kiuchumi. Hadi kufika kwenye Kisiwa cha Lampedusa wamekumbana
na vikwazo vingi; wamenyanyasika na kudhulumiwa njiani; wanaomba msaada kutoka katika
nchi mbali mbali ili waweze kuanza tena safari ya maisha yao, wakiwa na matumaini
mapya.
Wanatambua kwamba, Italia inabeba mzigo mkubwa wa wahamiaji kutoka
sehemu mbali mbali za dunia, lakini ikisaidiwa na kuwezeshwa, maisha ya wahamiaji
na wakimbizi yanaweza kuboreka zaidi, kuna haja ya kuwa na mshikamano!
Baba
Mtakatifu kabla ya kuhitimisha Ibada ya Misa Takatifu amewashukuru kwa mara nyingine
tena wananchi wa Kisiwa cha Lampedusa kwa mfano na ushuhuda wa upendo na ukarimu kwa
wakimbizi na wahamiaji. Anawataka waendelee kuonesha moyo wa ukarimu kwa wale wanaotafuta
kuboresha maisha yao, ili waweze kuonja ukarimu wao.