2013-07-09 09:32:47

"Niliguswa sana na ulemavu wa dada yangu aliyenyimwa nafasi ya kujiunga na utawa, leo hii mimi ni mtawa na daktari"


Dr. Rev. Sr. Sabina Patrick Mangi wa Shirika la Masista wa Theresa wa Mtoto Yesu, Jimbo Katoliki Iringa, Tanzania, katika mahojiano na Radio Vatican anasema kwamba, chimbuko la wito wake ni kutokana na dada yake mkubwa kukataliwa kujiunga na maisha ya kitawa kutokana na ulemavu.

Jambo hili lilimsikitisha sana na kubakiza chapa ya kudumu moyoni mwake, tangu alipokuwa mdogo. Alipohitimu shule ya msingi, aliwakumbusha wazazi wake nia yake ya kuwa mtawa, akakubaliwa. Alipoulizia Mashirika ya Kitawa, alijulishwa kuhusu Shirika la Theresa wa Mtoto Yesu, ambalo pia ni Jina la Mama yake, hapa akasema, amefika!

Leo hii ni daktari wa magonjwa ya binadamu, utume anaoutekeleza Jimboni Iringa. Familia yake ikabahatika pia kupata Padre, kumbe, Familia ya Mzee Petrick Mangi, ina Padre na Mtawa, matendo makuu ya Mungu katika hija ya maisha ya binadamu! Huu ni ushuhuda wa maisha na wito wa kitawa wakati huu, Mama Kanisa anapoadhimisha Siku ya Waseminari na Wanovisi, kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.

Anasema, kama Mtawa na Daktari katika maisha na utume wake anakumbana na changamoto mbali mbali, ambazo kimsingi ni nyingi, lakini anajitahidi kukabiliana nazo kadiri ya maisha na wito wake kama Mtawa na Daktari. Changamoto nyingi ni zile zinazoibuliwa kutoka katika maisha ya ndoa na familia; kanuni maadili, Mafundisho Jamii ya Kanisa kuhusiana na maisha ya ndoa na familia; Injili ya Uhai, Utu na heshima ya binadamu.

Uelewa na changamoto za kimaadili na kitaaluma katika kukabiliana na ugonjwa wa Ukimwi. Kuna haja kwa Kanisa kuendelea kuwaelimisha waamini wake kuhusu Mafundisho Jamii ya Kanisa na jinsi ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika maisha yao ya kila siku. Waamini wengi bado hawana ufahamu mkubwa kuhusu Mafundisho Jamii ya Kanisa, hali ambayo wakati mwingine inawafanya kuchukua maamuzi pengine kinyume cha Mafundisho na Msimamo wa Kanisa Katoliki.

Sr. Sabina anasema kwamba, hata vijana ni kundi ambalo linahitaji kusaidiwa kikamilifu kwani wanapambana na athari za utandawazi na mmong'onyoko wa maadili na utu wema. Kuna mambo mengi wanayoona na kujifunza kutoka katika mitandao ya kijamii na vyombo vya mawasiliano ya kijamii; mambo ambayo wakati mwingine yanasigana kabisa na: Imani, malezi, maadili, tamaduni bora za maisha ya Kitanzania na Kiafrika.







All the contents on this site are copyrighted ©.