2013-07-09 10:46:31

Gesi asilia inalenga kupambana na baa la umaskini Tanzania, ni kwa ajili ya mafao ya wote!


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa jukumu kubwa la gesi asilia nyingi iliyogunduliwa na inayoendelea kugunduliwa maeneo mbali mbali nchini ni kuwatoa Watanzania katika umaskini. Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa ni lazima wananchi waweze kuona na kuthibitisha manufaa ya gesi hiyo kwa maendeleo yao katika kipindi kifupi.

Pia Rais Kikwete amesema kuwa uchochezi wa baadhi ya wanasiasa kuhusiana na gesi asilia iliyogunduliwa nchini ni changamoto ambayo, hata hivyo, Serikali yake iko tayari kupambana nayo. Rais Kikwete alitoa msimamo huo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Kundi la Makampuni ya British Gas (BG) Bwana Chris Finlayson, moja ya makampuni ambayo yamegundua gesi na yameanza kuwekeza katika uchimbaji wa raslimali hiyo muhimu.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam, Rais Kikwete alimwambia Bwana Finlayson na ujumbe wake kuwa gesi asilia hiyo inayoendelea kugunduliwa nchini ni raslimali muhimu na lazima itumike katika “kuwatoa watu wetu katika umasikini na lazima ibadilishe maisha yao.” Aliongeza Rais Kikwete: “Hivyo, maandalizi ya uchimbaji wake yasichukue muda mrefu …..miaka 10 hivi….. huu ni muda mrefu sana kwa sababu wananchi wetu wanahitaji kuona manufaa ya gesi asilia hiyo katika kipindi kifupi iwezekanavyo”.

Aliongeza Rais Kikwete: “Ni dhahiri kuwa nyie wabia wetu mtanufaika na gesi asilia hiyo kutokana na uwekezaji wenu lakini kimsingi tunataka gesi hii iwanufaishe watu wetu, iwatoe katika umasikini. Kama gesi hiyo inaweza kutuingizia pato la dola za Marekani bilioni moja kwa mwaka, ni dhahiri tunaweza kuibadilisha nchi hii ikawa mbingu.”

Kuhusu wanasiasa wachochezi ambao wamekuwa wanawachochea wananchi wa Mtwara kudai kuwa gesi isitoke katika Mkoa huo na kuwa itumike kwa manufaa yao pekee, Rais Kikwete alisema:“Uchochezi wa wanasiasa ni changamoto. Hakuna shaka. Lakini hii ni changamoto ambayo Serikali itapambana nayo na ina uwezo wa kutosha wa kumaliza changamoto hiyo.”

Naye Bwana Finlayson alimweleza Rais maendeleo ya maandalizi ya uchimbaji wa gesi asilia hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa nafasi za masomo kwa vijana wa kitanzania kusomea utaalamu mbali mbali wa gesi hiyo asilia.

JK: Tutafuta aibu ya kuagiza siagi na jibini toka nje

Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali yake itaanza safari ya kufuta aibu ya Tanzania kuendelea kuagiza siagi na jibini kutoka nje ya nchi wakati kuna raslimali za kutosha kuzalisha bidhaa hizo hapa nchini. Hivyo, ameomba Uholanzi kushirikiana na Serikali ya Tanzania na wadau wengine nchini kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya mifugo na sekta ndogo ya uzalishaji maziwa, kama hatua ya kwanza kuachana na uagizaji wa bidhaa hizo ambazo zinaweza kuzalishwa nchini.

Rais Kikwete amesema kuwa sambamba na mageuzi katika sekta ya mifugo, Serikali yake inataka kuongeza kasi katika uwekezaji na uzalishaji wa maua na mazao mengine ya bustani hasa katika maeneo yenye hali ya hewa ya kustawisha mazao hayo kama Nyanda za Juu Kusini.

Rais Kikwete ameyasema hayo Jumatatu, Julai 8, 2013 Ikulu, Dar Es Salaam wakati alipokutana na Balozi wa Uholanzi nchini, Mheshimiwa Dkt. Ad Koekkoek ambaye amemaliza muda wake na alikuwa anamwaga Rais. Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete amemshukuru Balozi Koekkoek kwa “kuufikisha uhusiano wetu kwenye ngazi za juu kabisa za mahusiano ya kimataifa” na kumtaka aendelee kuunga mkono jitihada za maendeleo ya Tanzania popote atakapokuwa baada ya kustaafu.

Rais amemwambia Balozi kuwa Tanzania inataka kuendeleza sekta ya uzalishaji maziwa nchini na bidhaa zinazotokana na maziwa ikiwa ni pamoja na siagi na jibini. “Kuagiza siagi na jibini kutoka nje ya nchi ni jambo halina maelezo ya kutosha wala kuridhisha wakati tunazo raslimali zote za kutosha kuzalisha bidhaa hizo hapa nchini.”

“Tunataka kuleta mageuzi makubwa katika sekta hii na tunaomba Serikali ya Uholanzi kuwa mbia wetu mkubwa kwa sababu siyo tu kwamba ina uzoefu wa miaka mingi na ujuzi mkubwa wa eneo hili, lakini pia ni soko muhimu wa bidhaa za maziwa kama ilivyo soko la bidhaa za maua.”

Wakati huo huo, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Korea Kusini Mhe. Hee Chang na ujumbe wake. Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu, Dar Es Salaam. Katika mazungumzo hayo, Mheshimiwa Hee Chang amesifu mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Kikwete akisisitiza kuwa Tanzania ina nafasi ya kuweza kupiga hatua kubwa za maendeleo katika miaka ijayo kama itaendelea na kasi ya sasa ya maendeleo na kukua kwa uchumi.

“Miaka 50 iliyopita, Korea Kusini ilikuwa nchi masikini kabisa pato la wastani la kila Mkorea likiwa ni dola za Marekani 80 tu. Katika miaka 30 hadi 40, hata hivyo, tumefanikiwa kupiga hatua ya maendeleo na tuko tayari kutumia uzoefu wetu wa kukabiliana na changamoto za maendeleo kusaidiana na Tanzania, nchi ambayo ina kila dalili za kuleta mageuzi ya haraka katika kiwango chake cha maendeleo.” Amesema Spika huyo na kuongeza: “Tanzania ni mbia wetu wa kiuchumi na tunataka kusema kuwa kama mkikabiliwa na tatizo la kiuchumi ama la kimaendeleo ambalo tunaweza kulitatua kwa uwezo wetu mdogo, tunawakaribisha sana. Tuko tayari kushirikiana na kufanya kazi nanyi.”

Naye Rais Kikwete ameishukuru Korea Kusini kwa mchango wake katika maendeleo ya Tanzania katika nyanja mbali mbali ukiwamo ujenzi wa Daraja la Malagarasi (Daraja la Kikwete) ambao uko kwenye hatua za mwisho kukamilika. “Daraja lile ni ishara kubwa ya urafiki kati ya Tanzania na Korea Kusini. Ni daraja ambalo limefungua mawasiliano ndani ya nchi yetu na ni daraja ambalo limefungua mawasiliano kati ya Tanzania na nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC). Tunawashukuru sana.”











All the contents on this site are copyrighted ©.