Asante Papa Francisko kwa kuwa ni chombo cha amani, njaa na kiu ya watu wanaoteseka
na mawimbi mazito baharini!
Moyo wangu wamtukuza Bwana na roho yangu inamshangilia Mungu Mkombozi wangu, kwa kuwa
amewatembelea watu wake. Ni wimbo wa sifa na shukrani uliotolewa na Askofu mkuu Francesco
Montenegro, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Agrigento, Kusini mwa Italia, mara baada ya
Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko, kwenye
Kisiwa cha Lampedusa alikokwenda kusali na kutoa heshima kwa wahamiaji na wakimbizi
wanaopoteza maisha yao baharini wakiwa safarini kwenda Barani Ulaya.
Lampedusa
kimekuwa ni Kisiwa cha Matumaini na Kifo, kwani hapa kuna wakimbizi na wahamiaji kutoka
sehemu mbali mbali za dunia wanatia nanga ya matumaini kwa leo na kesho iliyo bora
zaidi. Ni mahali ambapo watu wanaonja adha ya utumwa, nyanyaso na madhulumu ya kila
aina, lakini bado wanapiga moyo konde kutafuta uhuru na maendeleo ya kweli, lakini
kwa bahati mbaya, wengi wao wanapoteza maisha wakiwa baharini hata kabla ya kufika
Kisiwani hapo.
Askofu mkuu Francesco Montenegro anasema, Kisiwa cha Lampedusa
ni mahali ambapo watu wanatafuta haki na utu wa mwanadamu unaopaswa kulindwa na kuheshimiwa.
Kuna haja ya kujenga utamaduni wa ukarimu, upendo na mshikamano wa kweli kwa nchi
hizi ambazo kwa miaka mingi zilitambulikana kuwa ni tajiri, lakini leo hii zinakumbana
na umaskini wa hali na kipato!
Waamini wa Jimbo kuu la Agrigento wanamshukuru
Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kuwa ni chombo cha amani na njaa pamoja na
kiu ya haki kwa wote wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia; hawa ni watu wanaopaswa
kuonjeshwa mawimbi ya upendo na ukarimu.