2013-07-08 11:54:49

Waseminari na Wanovisi wanapaswa kuwa ni wajumbe wa faraja, wanaobeba Msalaba wao kwa imani na matumaini katika sala na utume!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu, Jumapili, tarehe 7 Julai 2013, wakati wa kufunga Maadhimisho ya Siku ya Waseminari na Wanovisi, kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, amewapongeza vijana hao katika hija ya maisha inayowapatia fursa kugundua, kuhakiki na kuimarisha wito wao kwa njia ya majiundo makini.

Vijana hawa wanapaswa kutambua kwamba, wanaitwa na Kristo mwenyewe ili kushiriki utume wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya kumi na nne ya kipindi cha Mwaka wa Kanisa inakazia mambo makuu matatu: furaha katika faraja, Msalaba na umuhimu wa sala.

Baba Mtakatifu amewaambia Waseminari na Wanovisi waliofurika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwamba, hata katika mahangaiko yao ya ndani, Mwenyezi Mungu anaweza kuwakirimia faraja na kubembelezwa kama Mama mzazi afanyavyo kwa mtoto wake. Kila mwamini anaalikwa kuwa mjumbe wa matumaini kwa wale waliokata tamaa.

Ili kufanikisha utume huu, waamini wenyewe wanapaswa kuonja faraja na furaha inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Huu ndio utume ambao waamini wanapaswa kuutekeleza katika maisha yao kwa njia ya ushuhuda wa maisha yanayoburudisha mioyo ya wale waliokata tamaa, ili kuamsha tena matumaini mapya yanayopata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu amewaambia Waseminari na Wanovisi kuhusu umuhimu na ukuu wa Fumbo la Msalaba, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka katika wafu, kielelezo cha ushindi mkuu. Kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu, hata wao watakabiliana na Fumbo la Msalaba katika maisha na utume wao, utakaowawezesha kuzaa matunda yanayokusudiwa katika shughuli za kichungaji mintarafu mantiki ya Kristo mfufuka. Ni mwaliko wa kujitoa katika ubinafsi, tayari kujitosa kimasomaso kutangaza upendo wa Kristo. Msalaba wa Kristo ni kielelezo cha ushindi, huruma na upendo wa Mungu unaomwezesha mwamini kuwa ni kiumbe kipya.

Baba Mtakatifu anawaalika Waamini kusali bila kuchoka kwa ajili ya watenda kazi katika shamba la Bwana. Ni changamoto kwa watawa kujenga na kudumisha utamaduni wa kupenda kusali daima, kama alivyokazia Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita wakati wa utume wake. Utume ni matokeo ya sala, mwanga na nguvu ya kuweza kusonga mbele. Kanisa halitaweza kupata mafanikio makubwa ikiwa kama halitaweza kujishikamanisha na Kristo kwa njia ya sala na tafakari ya kina, chemchemi ya maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Uinjilishaji unafanyika kwa njia ya kupiga magoti, mwaliko kwa Waseminari na Wanovisi kuwa kweli ni watu wa sala, vingine utume wao utakuwa sawa na ajira zinazopatikana duniani. Yesu alikuwa ni mtu wa sala, daima alijitenga na watu akapata muda wa kusali kabla ya kufanya matukio makubwa katika maisha yake, changamoto endelevu kwa Mapadre na Watawa kujenga utamaduni wa kufanya tafakari ya kina na kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaongoza kwa mwanga wa Roho Mtakatifu. Msalaba uwe ni dira na mwongozo wa maisha na utume wao!







All the contents on this site are copyrighted ©.