Papa Francisko ni mjumbe wa amani, matumaini na mshikamano wa mapendo!
Askofu mkuu Francesco Montenegro wa Jimbo kuu la Agrigento lililoko Kusini mwa Italia
anasema, hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko ni tukio la furaha na neema
kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Uamuzi wa Baba Mtakatifu kutembelea na kusali na wananchi
wanaoishi katika Kisiwa cha Lampedusa ni ujumbe wenye nguvu na mwaliko wa kusoma alama
za nyakati kwa jicho la Kimungu.
Kisiwa cha Lampedusa kwa miaka mingi kimekuwa
ni alama ya matumaini kwa wahamiaji na wakimbizi kutoka Barani Afrika wanaotaka kusalimisha
maisha yao. Baadhi yao wanatafuta jinsi ya kuboresha maisha yao wakiwa Italia na Ulaya
katika ujumla wake.
Dhana ya uhamiaji inabeba ndani mwake anasema Askofu mkuu
Montenegro mateso na mahangaiko ya ndani; hiki ni kilio cha watu wanaotafuta haki
na amani. Kundi hili ni kubwa kiasi kwamba, watu hawawezi kukaa kimya kana kwamba,
hakuna kinachotendeka kwa maelfu ya watu wanaoendelea kuteseka na kufa maji baharini.
Uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko kisiwani hapa ni changamoto kwa wadau mbali
mbali kujifunga kibwebwe kwa njia ya msingi wa Injili, ili: uhuru, haki na amani viendelee
kutawala sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu anapenda kuwaimarisha waamini
katika kutekeleza wajibu wao wa Kikristo kwa kuwaonjesha jirani zao upendo na ukarimu.
Askofu mkuu Francesco Montenegro wa Jimbo kuu la Agrigento anasema kwamba,
waamini na watu wenye mapenzi mema Jimboni mwake, wamejiandaa kiroho na kimwili kwa
ajili ya hija ya mshikamano inayofanywa na Baba Mtakatifu Francisko Jimboni humo.