2013-07-08 07:27:58

Onesheni mshikamano wa upendo kwa wakimbizi na wahamiaji!


Haitoshi kuanzisha vituo maalum kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji sanjari na kufanya maboresho ya huduma msingi inayotolewa kwa watu hawa ambao mara nyingi wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha. RealAudioMP3

Jambo la msingi linasema, Shirika la Wayesuit kwa ajili ya kuhudumia Wakimbizi ni wananchi Barani Ulaya kufungua mioyo na akili zao, ili kuonesha mshikamano wa upendo na wakimbizi pamoja na wahamiaji, wanaohitaji kuonjeshwa kwa namna ya pekee faraja na huruma inayosimikwa katika utu na heshima ya binadamu. Bara la Ulaya likipania linaweza kutekeleza dhamana hii kwa kiwango cha hali ya juu kabisa!

Ni tafakari ya kina ambayo imefanywa na Shirika la Wayesuit kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi, wakati huu Baba Mtakatifu Francisko anapotembelea Kisiwa cha Lampedusa, Kusini mwa Italia, mahali ambapo kimekuwa ni kielelezo cha matumaini na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji hasa kutoka Barani Afrika. Wananchi wa Bara la Ulaya wanayo fursa na uhuru wa kuweza kutembea sehemu mbali mbali ndani na nje ya Bara la Ulaya. Hii inaonekana kwamba, inawezekana kutoa nafasi kwa watu wengine pia kuweza kushiriki katika uhuru huu.

Wakimbizi na wahamiaji ni watu wanaoendelea kutafuta mahali pa kuhifadhi maisha na utu wao kama binadamu, lakini bado wanakabiliana na vikwazo vingi. Taarifa ya hali ya wakimbizi Barani Ulaya inabainisha kwamba, wahamiaji waliomba hifadhi Barani Ulaya, bado wanataabika kupata malazi safi na bora; wengi wao hawana uwezo wa kupata tiba na huduma nyingine za kijamii na kwamba, wanashinda na njaa kwa mda mrefu.

Kuna baadhi ya miji ambamo sheria inaitaka miji hii kuhakikisha kwamba, inatoa makazi na malazi kwa watu hawa, lakini bado hali ni ya kutisha sana. Hawa ni watu wanaolazimika kulala kwenye Vituo vya Mabas na Treni. Ni watu wanaotanga tanga utadhani kwamba, “dala dala imekatika usukani”!

Takwimu za Bara la Ulaya zinaonesha kwamba, katika kipindi cha mwaka 2012, wahamiaji 102, 700 walipewa hifadhi katika nchi za Ulaya. Idadi hii inaweza kuonekana kuwa ni kubwa, lakini ukweli wa mambo hii ni asilimia 0.02% ya idadi ya wakazi wote wa Bara la Ulaya. Kuna sheria kali zinazosababisha mchakato wa wakimbizi na wahamiaji kupata vibali kuwa ni ngumu sana na wale wanaobahatika kuvipata, wanajikuta wakiwa wametengana na familia zao, hali inayoonesha kwamba, kuna udhaifu mkubwa katika sheria na taratibu za kupata hifadhi ya kisiasa.

Baadhi ya nchi zimejikuta zikiwaweka wahamiaji na wakimbizi vizuizini, hali inayoonesha jinsi ambavyo binadamu anavyoweza kunyanyasika na uhuru wake kubezwa na kutwezwa. Shirika la Wayesuit kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi, limejitahidi kurekebisha hali hizi, lakini bado kuna mambo mengi yanayopaswa kuboreshwa. Ziara ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko, kisiwani hapa iwe ni changamoto kwa wananchi wa Bara la Ulaya kuonesha mshikamano wa upendo unaoongozwa na kanuni auni.

Baada ya miaka mitano ya majadiliano ya kina, Mashirika ya Yasiyo ya Kiserikali yaliandika taarifa kwa pamoja kuunga mkono, baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Bunge hilo kuhusu hali ya wakimbizi kwa kuzingatia sheria zinazozingatia msingi wa kibinadamu. Lakini, kuna mambo yanayopaswa kufanyiwa marekebisho makubwa kuhusu sheria ili kukidhi mahitaji ya hifadhi ya wakimbizi na wahamiaji Barani Ulaya.

Mashirika haya yanasema kuna haja ya kubadili mfumo wa kuwaweka wakimbizi na wahamiaji kizuizini, mchakato uyaangalie makundi maalum pamoja kupata msaada wa kisheria. Mashirika haya nchini Ujerumani yanasema, kuna haja kwa Serikali za nchi za Ulaya kuonesha mshikamano pamoja na kushirikiana katika kubeba gharama za kuwahifadhi wakimbizi, hali ambayo wakati mwingine, inapelekea ongezeko kubwa la kodi.

Hali ya wakimbizi nchini Ugiriki, Italia, Hungaria na Malta ni tete kiasi kwamba, wakimbizi na wahamiaji wanalazimika kuishi vizuizini kwa muda mrefu, jambo ambalo ni kinyume kabisa cha sheria za kimataifa.

Mfumo wa sheria kwa sasa unawafanya wahamiaji na wakimbizi wengi kushambuliwa, kukosa malazi na hatimaye, kujikuta wakitumbukia katika umaskini. Wakimbizi walindwe na kupata hifadhi, kwani ni binadamu wenye heshima na hadhi yao! Wahamiaji wapewe fursa ya kuweza kuishi Barani Ulaya. Hii ndiyo hali halisi ambayo wakimbizi na wahamiaji wanakumbana nayo katika nchi mbali mbali Barani Ulaya.









All the contents on this site are copyrighted ©.