Kama Wamissionari pandikizeni mbegu ya: maisha, afya na faraja kwa wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 7 Julai
2013, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, aliwashirikisha
waamini furaha ya kukutana na kusali pamoja na Waseminari na Wanovisi kutoka sehemu
mbali mbali za dunia, katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.
Baba Mtakatifu
anawaalika waamini kusali na kuwaombea vijana hawa ambao wanajiandaa kuwa ni Mapadre
na Watawa, ili waweze kukua na kukomaza wito wao, ili hatimaye, waweze kuwa kweli
ni Wamissionari kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Anakumbusha kwamba, Yesu alikuwa
ni Mmissionari mahiri, lakini pia alipenda kuwashirikisha wafuasi wake katika kutangaza
Habari Njema ya Wokovu, huku wakiendelea kuwamegea watu upendo, umoja na mshikamano
wa watu wa Mungu.
Hiki ndicho kielelezo cha Jumuiya ya Kwanza ya Wamissionari
waliokuwa chini ya uongozi wa Kristo mwenyewe, akawafunda na kuwatuma ulimwenguni
kote! Hii ndiyo changamoto iliyoko mbele ya Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia
ya tatu ya Ukristo, muda unazidi kuyoyoma, kumbe, hakuna wakati wa kupoteza. Wagonjwa
wapate tiba kwani Mungu anataka kumponya mwanadamu kutoka katika mateso na mahangaiko
yake.
Huu ndio utume unaoendelea kutekelezwa na Wamissionari sehemu mbali
mbali za dunia, huku wakipandikiza mbegu ya maisha, afya na faraja kwa wale wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii. Hii ni changamoto kwa Wamissionari kujitoa bila ya kujibakiza
kwa ajili ya Mungu na jirani, jambo la msingi kwa vijana ni kujenga na kukuza ndani
mwao moyo, ari na ujasiri sanjari na kusikiliza sauti ya Kristo inayowaita kuwa ni
Wamissionari.
Baba Mtakatifu anasema kwamba, Wafuasi 72 waliotumwa na Yesu,
wanawawakilisha: Makleri, Watawa, Makatekista na Waamini walei wanaojitosa kutangaza
Injili ya Kristo kwa njia ya huduma: Parokiani, kwa wagonjwa, maskini na wote wanaoteseka;
wote hawa wanashiriki kujenga Ufalme wa Mungu, changamoto kwa kila mwamini kujisikia
kwamba, anao wajibu wa kuwa Mmissionari na kwamba, anatumwa kutangaza Habari Njema
ya Wokovu.
Wafuasi wale walipewa nguvu ya kumshinda Shetani, lakini Baba Mtakatifu
anakumbusha kwamba, mdau mkuu wa Uinjilishaji ni Kristo mwenyewe, wengine ni vyombo
vyake anavyovitumia, changamoto ya kumwomba Bikira Maria ili awaombee waweze kuwa
ni watangazaji bora wa Injili ya Kristo, wakiwa wamesheheni furaha na ujasiri!
Mara
tu baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Francisko aligusia Waraka wake
wa kichungaji, Lumen Fidei, Mwanga wa Imani, ulioanza kuandikwa na Baba
Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita kwa kufuata tema ya: upendo na matumaini,
yeye anahitimisha kwa kuongeza Imani. Hii ni zawadi kwa Familia ya Mungu inayoalikwa
kuzama katika mambo msingi ya imani ya Kikristo, ili iweze kuwasaidia kukabiliana
na changamoto katika ulimwengu mamboleo. Waraka huu ni nyenzo muhimu hata kwa wale
wanaomtafuta Mwenyezi Mungu na maana ya maisha.
Baba Mtakatifu Francisko anauweka
Waraka huu chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria, kielelezo makini cha imani,
ili aweze kuwasaidia waamini kuvuna matunda yanayokusudiwa na Kristo mwenyewe.
Baba
Mtakatifu ametambua uwepo wa Kikundi cha Mahujaji vijana kutoka Roma, kinachojiandaa
kwa ajili ya kwenda kwenye Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Rio de Janeiro,
Brazil. Amewahakikishia kwamba, hata Yeye mwenyewe anaendelea kujiandaa kikamilifu,
ili kwa pamoja waweze kufanya hija kwenye Siku kuu ya Imani.