Ajali barabarani ni kati ya vyanzo vikuu vya vifo na ulemavu miongoni mwa vijana wengi
Barani Ulaya. Ajali barabarani zinachangia kuharibika kwa haraka kwa vyombo vya usafiri
na miundo mbinu inayogharimu kiasi kikubwa cha fedha za walipa kodi.
Baraza la
Maaskofu Katoliki Hispania katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, linawaalika watumiaji
wa vyombo vya usafiri kuhakikisha kwamba, wanakuwa makini katika matumizi ya barabara
ili kulinda na kuokoa maisha, vyombo vya usafiri na miundo mbinu. Wanawauliza watumiaji
wa vyombo vya usafiri na barabara, “Je, unapoendesha ni mwanga gani unaokuongoza?
Imani inakuwajibisha katika kuendesha”.
Maaskofu Katoliki Hispania wanawakumbusha
waamini na wananchi kwa ujumla kwamba, wanapaswa kuongozwa na imani katika matumizi
bora ya vyombo vya usafiri, ili kuokoa, kulinda na kudumisha Injili ya Uhai; vyombo
vya usafiri pamoja na miundo mbinu.
Sehemu hii ya Ujumbe wa Baraza la Maaskofu
ni changamoto katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Kristofa, inayoadhimishwa
kila Mwaka ifikapo tarehe 7 Julai.
Watumiaji wa vyombo vya usafiri watambue
kwamba, vyombo vyao ni madhabahu ndogo inayobebea Injili ya Uhai wa mwanadamu, kumbe,
kwa jicho na fikara hizi za kiimani, wawe makini katika matumizi bora ya barabara.
Uinjilishaji mpya unawachangamotisha waamini kuhakikisha kwamba, imani inakuwa ni
dira na mwongozo katika hatua mbali mbali za maisha yao hapa duniani. Kila mtu anapaswa
kuwajibika kuhusiana na maisha yake mwenyewe na yale ya jirani zake mbele ya Mwenyezi
Mungu.
Watu wakumbuke kwamba, maisha ya mwanadamu ni zawadi kubwa kutoka kwa
Mwenyezi Mungu na kwamba, ni matakatifu yanapaswa kulindwa na kuendelezwa. Baraza
la Maaskofu Katoliki Hispania linaipongeza Serikali kwa kuchukua hatua za dharura
ili kupunguza idadi ya ajali barabarani nchini humo na kwamba, kwa miaka ya hivi karibuni
idadi ya ajali zimeendelea kupungua mwaka hadi mwaka.
Papa Paulo VI kunako
mwaka 1978, akiwa nchini Hispania, aliwataka watumiaji wa barabara kuwa na busara
sanjari na kuheshimu sheria za usalama barabarani; mambo msingi kwa watumiaji wa barabara.
Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linahitimisha ujumbe wake kwa Maadhimisho
ya Kumbu kumbu ya Mtakatifu Kristofa msimamizi wa wasafiri hapo tarehe 7 Julai 2013
kwa kuwaweka wote chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria, nyota ya wasafiri.