2013-07-06 14:26:46

Rais Carmona akutana na kuzungumza na Papa Francisko mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 6 Julai 2013 amekutana na kufanya mazungumzo na Bwana Anthony Thomas Aquinas Carmona wa Jamhuri ya Trinidad na Tobago.

Rais Carmona baadaye alikutana na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameandamana na Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Katika mazungumzo yao, viongozi hawa wawili wamegusia kuhusu mchango wa Kanisa Katoliki naotolewa kwa wananchi wa Trinidad na Tobago hasa katika sekta ya elimu, afya na huduma kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Ni matumaini ya viongozi hawa wawili kwamba, ushirikiano baina ya pande hizi mbili utaendelezwa kwa ajili ya mafao ya wengi.

Viongozi hawa wameguswa na matatizo yanayowakabili vijana hasa katika mapambano dhidi ya makosa ya jinai. Kwa pamoja wamekazia umuhimu wa majiundo kwa ajili ya mtu mzima: kiroho na kimwili pamoja na kulinda mazingira kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.







All the contents on this site are copyrighted ©.