2013-07-06 11:36:40

Papa kuongoza Ibada ya toba na maondoleo ya dhambi, Kisiwani Lampedusa!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kichungaji kwenye kisiwa cha Lampedusa, Kusini mwa Italia, anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuomba maondoleo ya dhambi. Hii ni Ibada inayoadhimishwa kwa ajili ya mahitaji maalum kama inavyoelekezwa kwenye Misale ya Kirumi.

Liturujia ya Neno la Mungu inakazia dhana hii, kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wale waliopoteza maisha yao wakiwa njiani kutafuta usalama na nafuu ya maisha kama wakimbizi na wahamiaji.

Baba Mtakatifu katika hija hii, anapenda kukazia kwa namna ya pekee kabisa, toba, ili kuomba neema na huruma ya Mungu katika maisha ya wakimbizi na wahamiaji. Baba Mtakatifu wakati wa Ibada ya Misa Takatifu, atatumia Fimbo iliyotengenezwa kutokana na mbao za mabaki ya Mashua za Wakimbizi na Wahamiaji zilizookolewa baada kuzama katika Kisiwa cha Lampedusa, kama hata rangi zake zinavyoonesha.

Fimbo hii ina alama ya Samaki na Mikate miwili, changamoto iliyotolewa na Yesu mwenyewe kwa wanafunzi wake, kuwalisha wale watu zaidi ya elfu tano waliokuwa wamekusanyika kumsikiliza kutwa nzima. Hapo Yesu aliweza kuonesha muujiza kwa kutumia ukarimu wa kijana aliyekuwa na Samaki wawili na Mikate mitano. Hii ni changamoto ya kuonesha na kuonjeshana ukarimu kwa kutumia hata kile kidogo ambacho Mwenyezi Mungu amewakarimia waja wake.

Wananchi wa Lampedusa wanachangamotishwa kuonesha moyo wa ukarimu na upendo kwa ndugu zao Wakimbizi na Wahamiaji wanaopambana na changamoto za maisha! Vifaa vya Ibada ya Misa Takatifu vitakavyotumiwa na Baba Mtakatifu Francisko ni mwaliko wa kutafakari Fumbo la Msalaba linalojionesha katika maisha ya wahamiaji na wakimbizi wanaokufa maji baharini! Kabla ya Baraka ya Mwisho, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Agrigento, atatoa Neno la shukrani kwa Baba Mtakatifu na baadaye kwa pamoja watasali Sala ya Malaika wa Bwana.







All the contents on this site are copyrighted ©.