Mmechaguliwa kwa jicho la Kristo, endeleeni kufundwa na Kristo pamoja na Kanisa lake!
Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kwanza wa kichungaji, Mwanga wa Imani
anasema, Maadhimisho ya Siku za Vijana Duniani ni mahali ambapo vijana wanapata fursa
ya kushuhudia imani kwa namna ya pekee kabisa na kwamba, hii ni changamoto kwao kuhakikisha
kuwa wanajitahidi kuiishi imani hii kwa ukamilifu mkubwa. Ni mwaliko wa kutafuta utakatifu
wa maisha!
Padre Beno
Michael Kikudo wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam katika mahojiano maalum na Radio Vatican,
wakati huu Waseminari na Wanavisi wanapoadhimisha Siku yao kama sehemu ya Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani anapenda kuwaangalisha vijana hawa kwamba, kuna changamoto kubwa
mbele yao, kwani mavuno ni mengi lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache.
Hata katika uhaba wa miito mitakatifu ndani ya Kanisa, Waseminari na Wanovisi
wanapaswa kuishi utakatifu wa maisha kwani huu ndiyo mwaliko wa kwanza kabisa. Vijana
watambue wajibu na dhamana iliyoko mbele ya maisha yao, jambo linalowachangamotisha
kuwa waaminifu, wakweli na wa wazi, mambo ambayo yanafumbatwa katika utakatifu wa
maisha.
Wanapaswa kujiandaa vyema kwa kukazia vipaumbele vinavyotolewa na
Mama Kanisa katika majiundo ya elimu dunia, maisha ya kiroho, kiutu na kichungaji.
Watambue kwamba, majiundo ni mchakato endelevu, wao wanapaswa kujenga utamaduni wa
kusikiliza kwa makini mintarafu mahitaji ya Kanisa, daima wakisoma alama za nyakati.
Wazame na kuchagua fungu lililo bora, tayari kuwashirikisha wengine. Waseminari na
Wanovisi watambue kwamba, wamechaguliwa kwa jicho la Kristo, waendelee kufundwa na
Kristo mwenyewe!