2013-07-05 07:57:40

Mwaka wa Imani: Siku ya Majandokasisi na Wanovisi


Kunako mwaka 1995 Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili aliridhia ombi lililotolewa na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makleri ya kuadhimisha katika kila Jimbo, siku maalum ya kuombea utakatifu wa Makleri. RealAudioMP3

Siku kuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ikatengwa rasmi kwa ajili ya kuombea utakatifu wa Mapadre. Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 1856 Papa Pio wa IX aliitangaza kuwa ni Siku kuu kwa ajili ya Kanisa zima.

Kardinali Mauro Piacenza, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makleri katika maadhimisho ya Siku kuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu aliwaandikia barua Waseminaristi akiwakumbusha umuhimu wa siku hii katika hija ya maisha yao majiundo yao ya Kipadre. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika kufunga Mwaka wa Mapadre aliwaandikia Waseminaristi barua ya kichungaji akiwaelezea umuhimu wa kipindi cha majiundo na mambo msingi ambayo walipaswa kuzingatia kwa wakati huu.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican katika Maadhimsiho ya Mwaka wa Imani kwa Waseminaristi na Wanovisi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, yatakayofanyika Jumapili tarehe 7 Julai 2013 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatica kwa ibada ya Misa Takatifu inayotarajiwa kuongozwa na Papa Francisko, inapenda kuwakumbusha kwa mara nyingine tena yale yaliyojiri kwenye barua ya Kardinali Mauro Piacenza kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya kuombea Utakatifu wa Mapadre kwa kutambua kwamba, utakatifu ni wito wa kwanza kwa kila mwamini, lakini kwa namna ya pekee, Makleri wanaoadhimisha Mafumbo ya Kanisa na kuwasindikiza waamini katika hija ya utakatifu wa maisha.

Baba Mtakatifu Francisko tangu mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ametoa mwaliko wa pekee kwa Mapadre kuwa ni wachungaji wema kwa Familia ya Mungu iliyokabidhiwa kwao, kwa njia ya upendo mkamilifu na majitoleo makuu yanayoimarishwa kwa njia ya uhusiano wa dhati na Yesu Kristo, anayewakirimia neema, nguvu na ari ya kuweza kukabiliana na changamoto za maisha. Kumbe, huu ni mwaliko wa kuwa ni wachungaji wema mintarafu maelekezo ya Kristo mwenyewe. Dhamana hii inapaswa kuanza kufanyiwa kazi wakati huu wa malezi na majiundo ya kipadre.

Wafuasi wa Kristo wanapaswa kutembea kwa kufuata nyayo zake, wakiwa wamesheheni neema na kuubeba Msalaba wa Maisha na wito wa Kipadre kwa furaha na uchangamfu wa ndani. Kwa kutembea na Msalaba wa Kristo wataweza kulijenga na kuliimarisha Kanisa la Kristo, kiasi hata cha kuweza kumshuhudia kwa njia ya maisha na matendo yao. Ni changamoto kwa Mapadre kuuishi wito wao wa Kipadre kama alama ya utume kwa Kristo na Kanisa lake; Kanisa ambalo ni mchumba mwaminifu wa Kristo.

Kardinali Mauro Piacenza anawaambia Majandokasisi kwamba, wito wao ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu wanaopaswa kuujenga na kuuimarisha kwa njia ya masomo, mifano na ushuhuda ya walezi wao, lakini zaidi kwa kumtegemea Kristo. Wanaitwa na Kristo ili kumtumikia Kristo na ndugu zao katika Kristo ndani ya Kanisa; wito unaohitaji ukarimu wa kibinadamu; kielelezo cha majadiliano endelevu kati ya mwamini na Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka.

Yesu Kristo kila wakati ameendelea kuita watu ili waweze kushiriki katika maisha na utume wake wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, wakijielekeza zaidi katika ujenzi wa ufalme wa Mungu. Hawa ni madaraja kati ya Mungu na watu wake; kati ya mbingu na dunia, dhamana wanayoitekeleza kwa njia ya Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa.

Kardinali Mauro Piacenza anawakumbusha Majandokasisi kwamba, wanaitwa katika maisha na utume wa Kipadre si kwa mastahili yao, ili waweze kuwa ni madaraja kati ya Mungu na Watu wake na hivyo kuwezesha mchakato wa hija ya ukombozi kutendeka kwa njia ya Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Watambue upungufu wao kama binadamu, lakini wameitikia wito huu kwa moyo wa ukarimu na furaha kubwa!

Majandokasisi wanapaswa kutambua kwamba, wanachangamotishwa na Baba Mtakatifu Francisko kuiishi imani yao katika ari na moyo wa ujana, kwani waswahili wanasema, “Ujana ni mali”. Kwa kuwa na mshikamano wa dhati na Kristo, moyo wa mwamini hauwezi kuzeeka wala kuchakaa kama kiatu cha raba!

Huu ndio ule moyo wanaopaswa kuuoneshwa katika maisha na utume wa Kipadre. Moyo ambao unatunzwa kwa: sala; tafakari na ukimya wa ndani unaomwezesha mtu kusikiliza sauti ya Mungu pamoja na kutekeleza majukumu aliyokabidhiwa kwake na Mama Kanisa. Vijana wawe tayari kusikiliza sauti ya Mungu anapobisha katika milango ya mioyo yao, wawe tayari kumfungulia kama alivyofanya Bikira Maria, ili waweze kuwa na furaha ya Kiinjili.

Waseminari wanaweza kukuza na kuimarisha wito wao kwa njia ya sala, licha ya kuwepo kwa mikakati ya kichungaji inayoichangamotisha Familia ya Mungu kusali kwa ajili ay kuombea miito, kwani mavuno ni mengi, lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, anakumbusha kwamba, wito ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu unaohitaji jibu la ukarimu wa kibinadamu unaowashirikisha watu wengi ndani na nje ya Kanisa.

Waseminari waoneshe ile nia njema iliyoko ndani mwao ya kutaka kushiriki katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Wanapaswa kuuheshimu na kuuthamini wito wao wa Kipadre na kwamba, walezi wanao wajibu wa kuonesha ushuhuda wa utakatifu wa maisha ya Kipadre. Seminari ni Jumuiya ya malezi ya Kipadre, mifano bora ni kikolezo kikubwa cha miito ya kipadre ndani ya Kanisa.

Vijana waone na kuguswa na maisha matakatifu ya Mapadre, ili nao waweze kujitosa kimasomaso kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Waseminari wakuze ndani mwao ari na moyo wa kuungana na Kristo kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, inayowaonjesha upendo na huruma ya Mungu. Wapate ushauri kutoka kwa Mababa wa maisha ya kiroho Seminarini wanaowaongoza hatua kwa hatua ili waweze kuijongea Altare ya Bwana.

Kardinali Mauro Piacenza anawaalika kwa namna ya pekee walezi waliopewa dhamana hii na Maaskofu wao kulea na kukuza miito ya Kipadre, watekeleze wajibu huu kwa ari na moyo mkuu, wakionesha ukarimu na ukweli katika kuamua hatima ya wito wa kijana anayetaka kuwa Padre. Ikumbukwe kwamba, Kanisa linahitaji Mapadre, wema na watakatifu; wakweli na waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake.

Walezi wasifanye haraka kuamua kuhusu wito wa kijana, wajipatie muda wa kuchunguza ili uamuzi wao uweze kuwa ni wa haki na busara kabla ya kumruhusu Jandokasisi kupewa Daraja Takatifu la Upadre. Vijana ambao hawana mwelekeo au wito wa Kipadre washauriwe kuanzisha mchakato mwingine wa maisha. Waseminari wanaalikwa kwa namna ya pekee kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, kama walivyokuwa Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu.

Barua hii imehaririwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.