Jimbo kuu la Dar es Salaam linamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa
ajili ya zawadi ya Mapadre wapya na wale wa Shirika la Wakarmeli na Wasalesiani wa
Don Bosco waliopewa Daraja Takatifu la Upadre, Ijumaa tarehe 5 Julai 2013 na Askofu
Msaidizi Titus Joseph Mdoe wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam. Ibada hii imefanyika kwenye
Parokia ya Mbezi Louis, Kanisa la Mtakatifu Peter Claver.
Padre Beno
Michael Kikudo wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam ambaye kwa sasa yuko kwenye hija ya maisha
ya kiroho Lourdes, Ufaransa kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, katika mahojiano
na Radio Vatican, anapenda kuchukua nafasi hii kuwakaribisha Mapadre wapya kwa moyo
na mikono miwili, kwani mavuno ni mengi lakini watenda kazi katika shamba la Bwana
ni wachache.
Jimbo kuu la Dar es Salaam kwa sasa lina jumla ya Parokia 77 zinazohitaji
kuhudumiwa kwa karibu zaidi. Mapadre wapya watasaidia mchakato wa kuhakikisha kwamba,
Familia ya Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam inapata huduma makini kwa wakati muafaka,
changamoto kwa Mapadre wapya ni kuanza maisha na utume wao kwa kujishikamanisha na
Kristo, bila kupunguza kasi!
Padre Beno Kikudo kwa namna ya pekee kabisa anayaelekeza
macho na matumaini yake kwa Mafrateri 10 walioingia katika nyumba ya malezi, Mtongani,
Jimbo kuu la Dar es Salaam tayari kuanza majiundo ya maisha na utume wa Kipadre. Anawaalika
vijana hawa wote "kugangamara" na kamwe wasirudi nyuma kwani Kanisa lina matumaini
nao!