Mahujaji kutoka Tanzania wanatembelea Roma, Lourdes na Nchi Takatifu
Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kufanya
hija ya maisha ya kiroho kama sehemu ya mchakato wa kujipatia neema na baraka zinazotolewa
na Mama Kanisa.
Padre Raymond
Saba, katibu mkuu, Idara ya Uchungaji, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika
mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kwamba, kuna mahujaji 41 kutoka Tanzania
wanaotembelea: Roma, Italia; Lourdes, Ufaransa na Nchi Takatifu.
Kundi hili
la mahujaji kutoka Tanzania linafanya hija mjini Roma kwa kuwa hapa ni Makao Makuu
ya Kanisa Katoliki, mahali ambapo kuna makubiri ya miamba wa imani, Mitume Petro na
Paulo, walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, changamoto na
mwaliko wa kuifahamu, kuiungama, kuiadhimisha, kuiishi na kuisali imani hii. Watanzania
hao wanatembelea Lourdes, Ufaransa kwani hii ni sehemu muhimu sana katika kukuza na
kuenea kwa Ibada ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.
Padre Raymond Saba
ambaye ndiye mkuu wa msafara huu kutoka Tanzania anasema, wanapenda kufanya hija Nchi
Takatifu kwani hapa ni chimbuko la Imani ya Kikristo. Hii ni hija ambayo itawachukua
takribani wiki mbili.