Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amecharuka na kuwakemea viongozi na watendaji
wakuu kwenye sekta ya pamba ambao wanawawonya wakulima wadogo kwa kuwazuia kutumia
kilimo cha mkataba kama njia ya uhakika ya kupata soko kwa zao hilo.
Ametoa
kauli hiyo Alhamisi, Julai 4, 2013 wakati akifungua Kongamano na Mkutano wa Kumi wa
Wadau wa Sekta Ndogo ya Pamba ulioanza leo kwenye Chuo cha Benki Kuu jijini Mwanza.
Mkutano wa siku mbili utamalizika kesho.
Alisema Chama cha Wakulima Pamba
(TACOGA) hakina budi kusimamia mapinduzi ya kilimo cha pamba nchini kama kweli kinataka
kuwasadia wakulima wadogo watoke hapo walipo na waboreshe maisha yao. “TACOGA na TCA
(Chama cha Wafanyabiashara ya Pamba) kaeni pamoja na mfanye tathmini ya uundwaji wa
taasisi hizi. Ni lazima muwe tayari kutetea maslahi ya wakulima wa zao hili na si
vinginevyo... kama hamuwezi kulifanya hili basi hamstahili kuwepo,” alisema huku akishangiliwa
na washiriki wa mkutano huo.
Waziri Mku alisema wadau wengi aliokutana nao
wamependekeza kilimo cha mkataba kiendelee baada ya mapungufu yaliyojitokeza kufanyiwa
kazi ikiwemo kutoa elimu ya mkataba kwa wadau wote na kusajili vikundi vya wakulima
ili vitambulike kisheria.
“Naamini kabisa kuwa utaratibu huu wa kilimo cha
mkataba, ukisimamiwa vizuri, utaleta mafanikio katika kuongeza tija; kuboresha ubora
na usafi wa pamba, na hivyo kuifanya pamba ya Tanzania kurudia sifa iliyokuwa nayo
ya kulipwa bei ya upendeleo (premium price), kuboresha huduma za ugani na kuzuia wakulima
wasiendelee kupunjwa kupitia mizani,” alisema.
Aliwataka viongozi na wadau
wengine waache kutetea maslahi binafsi katika jambo hilo na badala yake wazifanyie
kazi changamoto zilizojitokeza ili zirekebishwe. “Ninawasihi tutengeneze mazingira
ambayo yanampatia mkulima fursa ya kufikia uzalishaji mkubwa wenye tija ambao pia
unampa nafuu ya maisha. Naiagiza, Bodi ya Pamba isimamie sheria katika utekelezaji
wa kilimo cha mkataba,” alisisitiza.
“Kuna baadhi ya watu wenye uwezo wa kifedha
hawautaki utaratibu huu kwani wamezoea kuwakopesha wakulima kwa riba kubwa wakati
wa dhiki na kuja kuwadai wakishauza mazao yao... utaratibu huu unawapunguzia wateja
kwani wakulima sasa watakuwa na utaratibu mbadala wa kupata mikopo nafuu kupitia mfumo
huu wa kilimo,” alisema.
Waziri Mkuu alisema utaratibu wa kilimo cha mkataba
katika zao la pamba unatekelezwa kwa ridhaa ya wadau wenyewe wa pamba waliokaa katika
Mkutano wa Saba uliofanyika Juni 11, 2011 baada ya miaka mitatu ya ufanisi wa majaribio
katika Mkoa wa Mara, Wilaya ya Bariadi (Simiyu) na Wilaya ya Kibondo (Kigoma).
Alisema
kilimo hicho kinachosimamiwa na Tanzania Gastby Trust kupitia Program ya Kuendeleza
Kilimo cha Pamba na Viwanda vya Pamba (CTDP) hapa nchini kinaelezewa kudhoofishwa
na uwepo wa viongozi wachache katika maeneo yanayolimwa pamba wanaopinga au kuwashawishi
wakulima kuukataa mfumo huo kwa maslahi yao binafsi.
“Katika maeneo mengine
utakuta wakala wananunua pamba kutoka kwa wakulima waliokopeshwa pembejeo na CTDP
bila ya wao kuwasaidia wakulima kwa hali yeyote wakati wa kilimo hivyo kufanya mfumo
wa kurejesha mikopo hiyo uvurugike, na wakulima washindhwe kurudisha mikopo yao,”
aliongeza.
Alisema hali hiyo ilisababishwa kilimo cha mkataba kisimamishwe
katika msimu wa kilimo wa 2012/2013 na kuchangia kushuka kwa uzalishaji wa zao hilo.
Alisema
licha ya kuwa zao la pamba linalimwa katika mikoa takriban 15 hapa nchini, bado kilimo
cha zao hilo kinakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo tija ndogo katika uzalishaji
wa pamba ambapo sasa hivi wastani wa Taifa wa uzalishaji ni kilo 300 kwa ekari ikilinganishwa
na lengo lililowekwa la kufikia uzalishaji wa kilo 1,500 kwa ekari ifikapo mwaka 2015.
“Hali
hii inatokana na wakulima wengi kutozingatia kanuni bora za kilimo cha pamba, huduma
duni za ugani na utafiti, ukosefu wa pembejeo, mitaji na soko la uhakika wa zao hili
pamoja na zana duni za kilimo. Uhaba wa viwanda vya kutosha kuongezea pamba thamani
ni jambo ambalo pia linasababisha tuuze pamba ghafi katika soko la dunia ambalo bei
yake mara kwa mara haitabiriki,” aliongeza.
Alisema changamoto nyingine ni
bei ndogo ya pamba wanayopata wakulima kutokana na kuyumba kwa bei ya zao hilo
katika soko la dunia. Ili kuondokana na tatizo hili, alisema wadau wamependekeza
kuanzishwa kwa mfuko maalumu wa kufidia bei ya zao la pamba kwa wakulima pale bei
zinaposhuka katika soko la dunia (Price Stabilization Fund) pamoja na kuongeza viwanda
vya kuiongezea pamba thamani.
Waziri Mkuu aliwataka wadau wote wa pamba waendelee
kushirikiana na Serikali ili kwa pamoja waweze kuinua kipato cha wakulima. “Wadau
wa pamba, lazima tuwe na mtazamo wa upeo mpana na wa mbali kuhusiana na mustakabali
wa maendeleo ya sekta hii muhimu kwa wananchi wetu na kwa uchumi wa Taifa letu kwa
ujumla”, alisema.