Waziri mkuu wa Italia Bwana Enrico Letta akutana na kuzungumza na Papa Francisko!
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, 4 Julai 2013 amekutana na kuzungumza na Waziri
mkuu wa Italia Bwana Enrico Letta. Baada ya kuzungumza na Baba Mtakatifu, Waziri mkuu
alipata fursa ya kukutana na kuzungumza na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu
wa Vatican pamoja na Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi
za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.
Viongozi hawa wawili katika
mazungumzo yao, wamegusia kwa namna ya pekee, changamoto zinazoikabili Italia na nchi
za Ulaya katika ujumla wake pamoja na kuibua mbinu mkakati utakaoziwezesha nchi hizi
kulinda fursa za ajira hasa miongoni mwa vijana. Wamejadili kuhusu uhusiano uliopo
kati ya Familia za Wananchi wa Italia na Kanisa Katoliki katika ujumla wake na changamoto
ya kuendelea kudumisha amani na utulivu.
Baba Mtakatifu na Waziri mkuu wa Italia,
wamejadili pamoja na mambo mengine pia kuhusu masuala ya kimataifa sanjari na mageuzi
yanayoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia. Kwa pamoja wamekubaliana kwamba,
kuna haja kwa wadau mbali mbali nchini Italia kuendelea kushirikiana kwa ajili ya
ustawi na maendeleo ya wananchi wa Italia katika ujumla wake na kwa ajili ya mafao
ya Jumuiya ya Kimataifa.