Watetezi wa haki msingi za binadamu waomba adhabu ya kifo isitishwe nchini Nigeria
Taarifa kutoka nchini Nigeria zinaonesha kwamba, kuna jumla ya wafungwa 1,000 wanaosubiri
utekelezaji wa hukumu ya kifo. Hawa ni wale waliohukumiwa adhabu hii na utawala uliopita.
Kutokana na taarifa hii, Tume ya haki ya Umoja wa Afrika imeiomba Serikali ya Nigeria
kusitisha utekelezaji wa adhabu ya kifo, baada ya wafungwa wanne waliohukumiwa adhabu
hii kunyongwa hivi karibuni, hali ambayo iliibua shutuma kutoka ndani na nje ya Nigeria.
Wafungwa hao walinyongwa mara baada ya Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria kutia
sahihi hati ya kunyongwa kwa wafungwa watano, mmoja bado anasubiri utekelezaji wa
adhabu hii. Mwanasheria na mtetezi wa haki msingi za binadamu Femi Falana ametuma
ombi kwa niaba ya watetezi wa haki msingi za binadamu kutoka Nigeria ili kusitisha
adhabu ya kifo inayowakabili wafungwa wengine magerezani.