Wanawake wakiwezeshwa katika afya, elimu na uchumi, umaskini Barani Afrika utapewa
kisogo!
Dhamana ya ukuaji na maendeleo ya Bara la Afrika iko mikononi mwa wanawake wenye madaraka
Barani Afrika, ambao wanapaswa kuwa ni wadau wa mabadiliko ya dhati, kwa kuwajengea
wanawake wenzao uwezo katika masuala ya elimu, afya na uchumi.
Viongozi wanawake
wajisikie kwamba, wanalo jukumu la kusaidia mchakato wa kuleta mabadiliko na maendeleo
ya kweli kwa wanawake ili kujenga na kuimarisha taifa kwa leo na kesho yenye matumaini
makubwa zaidi. Hii ndiyo changamoto iliyoibuliwa na wake wa Marais zaidi ya kumi kutoka
sehemu mbali mbali za Bara la Afrika, katika Kongamano la Kimataifa lililoandaliwa
na Taasisi ya George W. Bush wa Marekani, inayopania kuwawezesha wanawake katika masuala
ya elimu, afya na uchumi.
Wake hao wa Marais walipata fursa ya kubadilishana
uzoefu na vipaumbele katika maisha yao, huku wakichangamotishana kusimama kidete kukabiliana
na changamoto pamoja na magumu yanayowasibu watu wao. Kama wake wa Marais wanaweza
kutumia ushawishi wao kukoleza maendeleo na kudumisha uhuru na demokrasia Barani Afrika.
Huu ni wito ambao umetolewa na Mama Laura Bush, mke wa Rais mstaafu wa Marekani, ambaye
amesema atendelea kuunga mkono juhudi za wanawake Barani Afrika katika elimu, afya
na uchumi.
Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania katika kongamano hilo amewakumbusha
wanawake kwamba, wao ni kiungo makini cha mchakato wa maendeleo katika Jamii na Taifa
katika ujumla wake. Wanawake ni wadau wakuu wa maendeleo, lakini ndilo kundi kubwa
katika Jamii linalokabiliana na umaskini kwani mara nyingi hlifaidi na kile wanachozalisha.
Hii ni changamoto ya kuondokana na mfumo dume ambao umekuwa ni chanzo cha
dhuluma na nyanyaso dhidi ya wanawake Barani Afrika. Wanawake wakiwezeshwa katika
afya, elimu na uchumi, umaskini Barani Afrika unaweza kupewa kisogo!
Mama
Michelle Obama amewataka wake wa Marais kutekeleza majukumu yanayogusa kwanza kabisa
mioyo yao, wajitoe kimasomaso kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa nchi zao pamoja
na kujiwekea mikakati watakayoitekeleza mara baada ya wanaume wao kuondoka madarakani;
mwaliko wa kuendelea kuwasaidia wanawake wenzao katika harakati za kujikwamua kiuchumi.
Kongamano hili la siku mbili limehudhuriwa na wake wa Marais kutoka sehemu
mbali mbali za Bara la Afrika pamoja na wake wa Mawaziri wakuu na viongozi wa wanawake
nchini Tanzania.