Rais Barack Obama wa Marekani amehitimisha ziara yake ya kikazi kwa nchi tatu za Kiafrika,
yaani Senegal, Afrika ya Kusini na Tanzania, ambako waswahili wanasema, eti, "amefunika".
Kati ya mambo ambayo yanaendelea kupewa kipaumbele cha pekee na uongozi wa
Rais Obama ni uhakika wa usalama wa chakula ili kupambana na baa la njaa linaloendelea
kutesa mamillioni ya watu duniani; afya: kwa kupambana na ugonjwa wa Ukimwi na maboresho
katika huduma ya nishati ya umeme, ili Bara la Afrika liweze kucharuka katika maendeleo,
hatimaye, liweze kuondokana na umaskini.
Katika mapambano dhidi ya baa la njaa,
Serikali ya Marekani kuanzia mwaka 2010 imechangia kiasi cha dolla billioni 3.5 ambazo
zimesaidia kuokoa maisha ya watu wengi Barani Afrika. Marekani itatoa kiasi cha dolla
billioni 7 kwa ajili ya nishati ya umeme. Rais Obama anaendelea kuwachangamostisha
Marais wa Afrika kusimama kidete kulinda na kudumisha utawala bora, demokrasia pamoja
na kung'oa vitendo vya rushwa na ufisadi ambavyo ni kizingiti kikuu cha maendeleo
Barani Afrika.
Rais Obama amewahakikishia wananchi wa Kenya kwamba, wao ni
sehemu ya moyo wake na kwamba, iko siku atawatembelea, pengine kwa sasa hali ya hewa
bado si shwari sana! Rais Obama amewaalika Marais wa Afrika hapo mwakani, kuhudhuria
mkutano unaopania kuimarisha urafiki kati ya Marekani na Afrika katika mchakato wa
maendeleo endelevu, kwani wakati wa kutoa hotuba nzuri umekwisha, sasa watu wanataka
kuona vitendo!