Vyombo vya habari viwe ni madaraja ya uhusiano mwema kati ya watu!
Baba Mtakatifu Francisko amekipongeza Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV kwa jitihada
zake za kuhakikisha kwamba, kinaendelea kuwa ni daraja kati ya Vatican na watu kutoka
sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu ameyasema hayo hivi karibuni mara baada
ya Kituo cha Televisheni cha Vatican kuwekeana mkataba wa ushirikiano na Kituo cha
Televisheni cha “Channel 21”.
Wananchi wa
Italia na Ulaya kwa ujumla watakuwa na fursa ya kuweza kufahamu hali halisi ya maisha
na utume wa Kanisa Bueno Aires. Hii ni kutokana na ushirikiano wa Kanisa Katoliki
nchini Italia kwamba, Kituo cha Televisheni cha Jimbo, kinaweza kurusha matangazo
yake kwa umati mkubwa zaidi, ili kuweza kufahamu utume na maisha ya Kanisa kutoka
sehemu mbali mbali za dunia. Kwa njia hii, watu wataweza kufahamiana na hatimaye,
kubomoa kuta za utengano, ambazo mara nyingi zimekuwepo kati ya watu wa mataifa.
Itakumbukwa
kwamba, Kituo cha Televisheni cha Channel 21, kinamilikiwa na kuendeshwa na Jimbo
kuu la Buenos Aires na kilianzishwa na Kardinali Jorge Mario Bergoglio kunako mwaka
2004. Baba Mtakatifu ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa anazungumza na Monsinyo
Dario Viganò, Mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Televisheni cha Vatican.
Akizungumza
katika hafla ya kuwekeana mkataba kati ya Kituo cha Televisheni cha Vatican na Kituo
cha Televishen cha Channel 21 mjini Vatican, Askofu mkuu Claudio Maria Celli anasema,
hizi ni juhudi zinazofanywa na CTV kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Miaka
thelathini tangu kilipoanzishwa. Ni kituo ambacho kimekuwa kikirusha picha za Mababa
Watakatifu: Yohane Paulo wa pili, Benedikto wa kumi na sita na sasa Papa Francisko.
Kituo
hiki kinaendelea kuhariri na kuhifadhi picha zote zilizopigwa na Channel 21 wakati
wa uongozi wa Kardinali Bergoglio, Jimbo kuu la Buenos Aires, Argentina. Kazi hii
inaunganisha pia picha zote za Kardinali Bergoglio hadi tarehe 13 Machi 2013, ambazo
zitawekwa katika mfumo wa dijitali.
Hifadhi ya picha hizi inafanikishwa na
mradi mkubwa wa Chumba cha kuratibu matangazo, ambacho kwa sasa kina uwezo mkubwa.
Chombo hiki kimenunuliwa kutoka kwenye Kampuni ya Sony. Kumbe, hakutakuwa na haja
tena ya kutumia mfumo wa picha ambazo zilikuwa zimehifadhiwa kwenye Kanda.
Channel
21, tangu kilipoanzishwa, kimekumbana na changamoto mbali mbali katika kuandaa na
kurusha vipindi vyake kwa umati mkubwa zaidi wa wananchi wa Argentina. Viongozi wa
Channel 21 kutoka Argentina waliohudhuria katika halfa ya kuwekeana mkataba na Kituo
cha Televisheni cha Vatican wanasema, Kardinali Jorge Mario Bergoglio, si mshabiki
sana wa masuala ya Televisheni, lakini tangu mwanzo alitambua umuhimu wake katika
mchakato mzima wa Uinjilishaji wa mtu mzima: kiroho na kimwili.
Akajifunga
kibwebwe kuwekeza katika uanzishwaji wa kituo hiki, leo hii kina mafanikio makubwa.
Alitamani kujenga na kuimarisha Kanisa, linaloshirikisha tunu msingi za maisha ya
Kikristo, kiutu na kimaadili.
Kwa njia hii, kadiri ya mawazo ya Kardinali
Bergoglio, Televisheni ilikuwa na wajibu wa kuwaendea watu waliokuwa pembezoni mwa
Jamii, ili kuweza kuwashirikisha ile furaha ya Ujumbe wa Neno la Mungu