Kwa sababu uhai wa binadamu ni mtakatifu, Tangu mwanzo wake, unahusisha tendo la Mwenyezi
Mungu la kuumba na unabaki daima katika uhusiano wa pekee na Muumba, aliye lengo lake
kuu. Kakuna anayeruhusiwa kuangamiza maisha ya mtu kwani. Hili ni tendo zito linalopingana
na hadhi ya mtu na utakatifu wa mwenyezi Mungu. Wasio na hatia na wenye haki usiwauwe.
Hivi
ndivyo Katekesimu Mpya ya Kanisa Katoliki inavyofundisha na kuendelea kukazia kwamba,
adhabu inayotolewa na mamlaka halali ya nchi inalenga kurekebisha vurugu iliyotokana
na kosa, kulinda utaratibu wa jamii na usalama wa watu, pamoja na kumsaidia mkosefu
kujirudi.
Adhabu inayotolewa inatakiwa ilingane na uzito wa kosa. Siku hizi
kutokana na Serikali kuwa na njia za kuzuia makosa ya jinai kwa kumfanya mkosefu asiweze
kudhuru, kesi ambazo zinahitaji kabisa adhabu ya kifo "zimekuwa nadra sana, au karibu
hazipatikani. Pale ambapo njia ya kutomwaga damu zinatosha, mamlaka iridhike nazo,
kwa kuwa zinaendana vizuri zaidi na hali halisi ya ustawi wa jamii. Zinalingana zaidi
na hadhi ya binadamu, tena hazimnyimi moja kwa moja nafasi ya kujirekebisha.
Ni
kutokana na Mafundisho haya ya Kanisa, Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria, hivi karibuni
limelaani kitendo cha Serikali kutekeleza adhabu ya kifo, iliyotokea mjini Benin
kuwa ni kitendo cha kinyama dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Tangu mwaka 2006
kumekuwepo na mchakato wa kufuta adhabu ya kifo nchini Nigeria, mchakato ambao kwa
sasa umevurugwa kutokana na Serikali kuamua kutekeleza adhabu ya kifo kwa wafungwa
wanne, hapo tarehe 24 Juni 203.
Askofu mkuu Ignatius Kaigama, Rais wa Baraza
la Maaskofu Katoliki Nigeria anasema, hadi sasa adhabu ya kifo inatajwa kwenye Katiba
ya nchi, jambo ambalo linapaswa kurekebishwa ili kulinda na kudumisha uhai wa mwanadamu
ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baraza la Maaskofu linaiomba Serikali
kuanzisha mchakato wa kufanya marekebisho ya dhati katika Katiba ili kuondokana na
sheria ambazo zinakiuka haki msingi ya mwanadamu, yaani uhai. Adhabu ya kifo imepitwa
na wakati kwani haitoi haki kwa mtuhumia kujirekebisha kwa siku za usoni.
Baraza
la Maaskofu Katoliki Nigeria linaiomba Serikali kuhakikisha kwamba, inaibua mbinu
mkakati utakaowawezesha wafungwa kujirekebisha na hatimaye, kuwa ni raia wema mara
baada ya kutumikia vifungo vyao. Leo hii kuna idadi kubwa ya nchi ambazo zinaendelea
kufuta adhabu ya kifo kwa raia wake. Lakini watuhumiwa wa makosa mbali mbali wanaendelea
kunyongwa nchini China, Iran, Iraq, Falme za Kiarabu na Marekani.