2013-07-02 08:53:50

Marekani na Tanzania zinapania kuimarisha ushirikiano wa kibiashara!


Rais Barack Obama wa Marekani katika ziara yake ya kikazi nchini Tanzania, ameipongeza Tanzania kwa kutumia vyema misaada inayotolewa na Marekani kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania hususan katika ujenzi wa miundo mbinu ya barabara;afya, maji, uzalishaji na usambazaji wa nishati ya umeme.

Kwa sasa Marekani inapenda kujielekeza zaidi katika uhusiano wa kibiashara kwa kujenga miundo mbinu na mapambano dhidi ya ujangiri kwenye mbuga za wanyama ili kukuza na kuimarisha sekta ya utalii nchini Tanzania. Taarifa ya Ikulu ya Marekani inabainisha kwamba, kiasi cha dolla za Kimarekani millioni 10 kitatolewa kwa ajili ya kupambana na ujangiri kwenye mbuga za wanyama nchini Tanzania.

Kwa upande wake, Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania ameishukuru Marekani katika kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi; maboresho katika sekta ya elimu, maji na nishati. Kwa sasa watumiaji wa nishati ya umeme wameongezeka kutoka asilia 10% hadi kufikia asilimia 21%. Miundo mbinu ya barabara imeboreka maradufu kiasi cha kuweza kuunganisha sehemu kubwa ya Tanzania.







All the contents on this site are copyrighted ©.