Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Kenya linaendelea kufanya tafakari ya kina kuhusu
hali ya maisha ya wananchi wa Kenya kadiri ya uongozi mpya. Maaskofu wanaipongeza
Serikali kwa kuleta mabadiliko makubwa mintarafu Katiba Mpya ambayo kimsingi ni sheria
mama, kwa kugawa madaraka mikoani, ili kupeleka huduma makini karibu na wananchi,
jambo ambalo ni la kwanza katika historia ya Kenya.
Maaskofu Katoliki Kenya
wanaonya kwamba, kumeibuka wimbi kubwa la rushwa, ufisadi, upendeleo na uongozi duni;
mambo ambayo pengine Serikali kuu haijayafanyia kazi vya kutosha. Kuna baadhi ya viongozi
wa kisiasa wametawaliwa mno na ubinafsi kiasi cha kushindwa kuona vipaumbele vya kitaifa,
kwa ajili ya mafao ya wengi, maendeleo na ustawi wa wananchi wa Kenya. Kuna baadhi
ya mambo kwenye bajeti ya mwaka si ya msingi, lakini yapo kwa ajili ya masilahi ya
baadhi ya watu ndani ya Jamii ya Wakenya.
Maaskofu Katoliki wanawataka wananchi
wa Kenya kuiwajibisha Serikali yao kwa kuhakikisha kwamba, inatumia vyema rasilimali
na mapato ya nchi kwa ajili ya mafao ya wengi. Kanisa kwa upande wake, litaendelea
kuwa ni mdau na mshiriki mkuu katika mchakato wa kuwaletea wananchi wa Kenya maendeleo
endelevu.
Hii ni changamoto kwa Serikali kuhakikisha kwamba, inaweka miundo
mbinu itakayowawezesha wananchi wengi kushiriki katika kupanga, kuamua na kutekeleza
maamuzi mbali mbali. Haya yamo kwenye taarifa ya Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya
kwa vyombo vya habari, baada ya kuzindua jina jipa la Baraza la Maaskofu Katoliki
Kenya.
Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasikitishwa na kinzani na migogoro
inayoendelea kujitokeza wakati wa vikao vya Bunge la Kenya na Baraza la Senate. Maaskofu
wanayaalika Mabaraza haya mawili kushirikiana katika maboresho ya huduma kwa wananchi
wa Kenya badala ya kupimana misuli, jambo ambalo halina tija wala mashiko kwa ustawi
na maendeleo ya wananchi wa Kenya.
Maaskofu wanaipongeza Serikali ya Kenya
kwa sheria ya elimu ya mwaka 2013 kuhusu elimu ya msingi na kwamba, Kanisa limekuwa
ni mdau mkuu katika huduma ya elimu kabla ya uhuru na sasa linaendelea kujitanua kwa
viwango na ubora. Maaskofu wanasema, shule zinazomilikiwa na Kanisa zina haki ya kumiliki
maeneo yale, ingawa baadhi ya vifungu vinasema kwamba, zimejengwa katika maeneo ya
Serikali. Umiliki wa ardhi unaofanywa na taasisi za kidini unapaswa kuheshimiwa kadiri
ya Katiba ya nchi.
Maaskofu Katoliki Kenya wanasikitishwa na mfumuko wa bei
ya bidhaa na huduma kutokana na ongezeko la thamani kama inavyooneshwa kwenye sheria
ya mwaka 2013. Licha ya kuongeza bajeti na makusanyo ya kodi ya Serikali, lakini Serikali
inapaswa kutambua kwamba, wananchi wake wengi ni maskini, hawana fursa za ajira na
wala hawana kipato cha uhakika! Serikali inawajibu wa kimaadili wa kuhakikisha kwamba,
wananchi wanaweza kumudu gharama ya maisha kwa kujipatia mahitaji msingi, yaani: chakula,
mavazi na malazi.
Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasikitishwa na tofauti
kubwa ya nyongeza za mishahara miongoni mwa wafanyakazi wa Serikali na wanataaluma.
Malumbano ya mishahara minono yanaweza kulitumbukiza taifa katika maafa makubwa na
hivyo Kenya kushindwa kutawalika.
Hii inatokana na ukweli kwamba, walimu wanaendelea
na mgomo kwa zaidi ya mara saba, hali ambayo ina dhohofisha sekta ya elimu nchini
Kenya na maendeleo ya wanafunzi.
Ni kweli kwamba, walimu wanayo haki ya kufanya
mgomo, lakini wanapaswa kutambua kwamba, ualimu ni wito na wanafunzi wana haki ya
kusoma. Hapa kuna haja kwa Serikali na walimu kufanya majadiliano ya kina ili kuweza
kupata ufumbuzi wa kudumu, anasema Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Kenya.
Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linahitimisha taarifa yake
kwa vyombo vya habari kwa kuwataka waamini kujenga na kuimaarisha moyo wa kimissionari,
kwa kuwapenda na kuwathamini jirani, daima wakisukumwa na ari pamoja na moyo wa upendo
na mshikamano kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kama
walivyofanya Watakatifu Petro na Paulo, miamba ya imani.