2013-06-29 11:26:48

Salini zaidi ili Majimbo tupu nchini Tanzania yapate wachungaji wake wakuu!


Chama cha Utoto Mtakatifu Jimbo kuu la Dar es Salaam hivi karibuni kilihitimisha kongamano lililowakusanya watoto kutoka katika Majimbo yanayounda Jimbo kuu la Dar es Salaam Jimboni Ifakara. Katika kongamano hilo watoto walipata fursa ya kufanya tafakari ya kina hasa wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, sanjari na dhamana ya wazazi na walezi katika malezi na makuzi ya watoto wao!

Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, aliwataka watoto kusali kwa ajili ya kuwapata wachungaji wakuu kwa Majimbo matano ambayo yamekuwa wazi kutokana na sababu mbali mbali. Kardinali Pengo anasema, majimbo haya kwa sasa ni mzigo mkubwa kwa Kanisa la Tanzania. Majimbo ambayo hadi sasa yako wazi ni: Jimbo kuu la Songea, Jimbo Katoliki la Shinyanga, Jimbo Katoliki la Kigoma, Jimbo Katoliki la Singida na Mpanda.

Kardinali Pengo katika Ibada ambayo ilihudhuriwa pia na Maaskofu wanaounda Jimbo kuu la Dar es Salaam aliwaambia watoto kusali zaidi kwani wao wanasikilizwa na Mwenyezi Mungu ikilinganishwa na watu wazima ambao wana dhambi nyingi. Watoto ni wanyofu mbele ya Mungu na kwamba, sala zao ni sawa na ubani mbele ya Mwenyezi Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.