Mshikamano wa upendo na Wananchi wa Amerika ya Kusini
Mfuko wa Maendeleo ya Watu "Populorum Progressio" uliohitimisha mkutano wake wa Mwaka
hivi karibuni huko Arequipa, nchini PerĂ¹ na kuhudhuriwa na Kardinali Robert Sarah,
Rais wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum, umekuwa
ni kielelezo makini cha alama ya mshikamano wa upendo na wananchi wanaoishi Amerika
ya Kusini.
Wajumbe wamechambua na kupitisha miradi mia mbili tu ambayo inapaswa
kuwa kweli ni alama ya upendo na mshikamano kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, kwa
ajili ya wananchi wenye asili ya Kiafrika wanaoishi Amerika ya Kusini. Baada ya kufanya
upembuzi wa kina anasema Monsinyo Segundo Tejado Munoz, Katibu mkuu mwambata wa Baraza
la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum, miradi 170 tu ndiyo ambayo
imeamriwa kwamba, itagharimiwa na mfuko wa Maendeleo ya watu kutokana na kipaumbele
na unyeti wake kwa sasa. Hii inatokana na ukweli kwamba, bado athari za myumbo wa
uchumi kimataifa zinaonesha makali yake!
Miradi mingi iliyopitishwa inapania
kuinua hali ya maisha, ustawi na maendeleo ya wakulima wadogo wadogo, ili waweze kuboresha
hali ya maisha yao na kuchangia ustawi wa familia zao katika ujumla wake. Kimsingi
hii ni miradi ya: kilimo, afya, elimu na maendeleo endelevu. Lakini, wajumbe kwa mwaka
huu wameguswa zaidi na miradi inayoangalia mahangaiko ya ndani ya mwanadamu, yaani
miradi inayopania maboresho ya huduma za kichungaji. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto
wa kumi na sita, aliwahi kusema kwamba, watu wanakabiliana na mateso makubwa si tu
kwa kukosa vitu bali kwa kutotambua na kuthamini uwepo wa Mungu katika hija ya maisha
yao!
Itakumbukwa kwamba, miradi mingi inayohudumiwa na Mfuko wa Maendeleo ya
watu inagharimiwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Kuna haja kwa waamini na
watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kuonesha ukarimu zaidi kwa Baba Mtakatifu
Francisko ili aweze kuwahudumia watu wengi zaidi wanaohitaji msaada wa hali na mali
huko Amerika ya Kusini.
Monsinyo Segundo Tejado Munoz anasema, Mkutano wa
Mfuko wa Maendeleo ya Watu kwa ajili ya Amerika ya Kusini, umegusia kwa namna ya pekee,
changamoto inayoendelea kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika kuwahudumia maskini
na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Ni kiongozi aliyeonja shida na mahangaiko
ya watu wake, ndiyo maana hapo mwakani, wajumbe watafanya mkutano wao wa mwaka mjini
Roma, ili waweze kupata nafasi ya kusikiliza changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu
Francisko kwa wakati huu.
Mfuko wa Maendeleo ya Watu unaendelea kufanya maboresho
katika huduma zake kwa kufanya tafiti kuhusu maisha ya watu mahalia, matatizo, changamoto
na fursa zinazopatikana katika maeneo yao, ili kuweza kuwashirikisha kikamilifu katika
huduma kwa maskin na hasa wale wanaoishi pembezoni mwa Jamii.
Kuna maendeleo
makubwa katika miji, lakini pia maendeleo haya yanaendelea kujenga pengo kati ya maskini
na matajiri na kwamba, kuna kundi la watu wengi wanaoishi katika hali ya umaskini
wa hali na kipato! Wote hawa wanahitaji kupewa ujumbe wa matumaini kwa wale wanaoishi
na wale ambao wako nje ya Kanisa. Upendo na mshikamano vinapaswa kuchukua kasi ya
pekee wakati huu watu wanapokabiliwa na athari za myumbo wa uchumi kimataifa! Watu
wasikate wala kukatishwa tamaa, waendelee kuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo
bora zaidi!