2013-06-29 10:25:54

Maaskofu Katoliki nchini Kenya wazindua mpango mkakati wa miaka 10! Wabadili Jina!


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya limezindua mpango mkakati wa miaka kumi utakaotekeleza utume na mwono wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya pamoja na kubadili jina kutoka katika jina lililokuwa limezoeleka kama "Kenya Episcopal Conference" (KEC) na sasa litajulikana kama " Kenya Confrence of Catholic Bishops (KCCB).

Akizungumza katika halfa hii, Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki wa Kenya anabainisha kwamba, mabadiliko ya jina yanapania kwa namna ya pekee kuhakikisha kwamba, wanatumia fursa hii kwa ajili ya ushuhuda wa utakatifu wa maisha; utekelezaji wa mikakati na shughuli za kichungaji mintarafu vipaumbele vya Kanisa Katoliki nchini Kenya.

Mabadiliko ya jina ni kutokana na kuibuka pia kwa Makanisa yenye majina kama haya, hali ambayo inaweza kuvuruga utambulisho wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya. Kardinali Njue anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya nchi yao, lakini zaidi watalaam na wanasiasa kuhakikisha kwamba, wanatekeleza majukumu ya kazi zao kwa ajili ya mafao ya wananchi wa Kenya na wala si vinginevyo.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya ni chombo kinachowaunganisha Maaskofu Katoliki wanaotekeleza dhamana ya kichungaji katika Kanisa Katoliki nchini Kenya, kwa kusoma alama za nyakati pamoja na kutekeleza utume wao mintarafu sheria, ustawi na maendeleo ya Kanisa na Kenya katika ujumla wake. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linaundwa na Maaskofu wa Majimbo Katoliki Kenya, Askofu wa Jimbo la Kijeshi, Wasimamizi wa kitume, Maaskofu waandamizi, Maaskofu wasaidizi pamoja na Maaskofu wenye dhamana ya kitume nchini Kenya.







All the contents on this site are copyrighted ©.