2013-06-29 14:28:49

Kanisa la Roma limejengwa katika msingi wa ushuhuda wa Mitume Petro na Paulo!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Maadhimisho ya Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani anasema, hii pia ni Siku kuu ya Jimbo kuu la Roma ambalo limejengekwa katika ushuhuda wa kifo dini cha Mitume hawa wawili.

Hii ni Siku kuu kubwa kwa Kanisa zima kwani Mitume hao wamekuwa ni chemchemi ya zawadi ya imani. Mtakatifu Petro alikuwa ni mtu wa kwanza kuungama kwamba, Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu aliye hai. Mtume Paulo, Mwalimu wa Mataifa akautangaza na kuueneza ujumbe huu kwa Wagriki na Warumi. Wote wawili wakayamimina maisha yao kwa ajili ya Imani kwa Kristo na Kanisa lake hapa mjini Roma. Kwa nguvu ya ushuhuda wa imani na upendo wao kwa Kristo ndio ulioibua imani na kuliendeleza Kanisa.

Mtakatifu Petro aliweza kutoa jibu makini kuhusu Umungu wa Kristo kwa vile alikirimiwa neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si kwa nguvu wala jeuri yake binafsi. Aliona, akasikia na kuguswa na ule upendo wa Mungu uliokuwa unatenda kazi ndani ya Kristo. Mtume Paulo, katika ujana wake anasema Baba Mtakatifu Francisko, aliwatesa na kuwadhulumu Wakristo, lakini tangu siku ile alipokutana na Yesu Mfufuka akiwa njiani kwenda Damasko, maisha yake yakabadilika, akawa ni mtu mpya.

Mtakatifu Paulo alitambua kwamba, Yesu alikuwa hai, alimpenda hata yeye mwenyewe ingawa alikuwa ni adui wake mkubwa. Hapa mwamini anaonja huruma na msamaha wa Mungu kwa njia ya Kristo. Hii ndiyo Habari Njema ya Wokovu, Injili ambayo imegusa maisha ya Watakatifu Petro na Paulo, kiasi cha kuyamimina maisha yao bila hata ya kujibakiza. Kuna neema na baraka kwa mwamini kuonesha imani yake kwa Mungu ambaye ni upendo mkamilifu.

Hii ndiyo imani iliyoungamwa na Mitume Petro na Paulo, waliyoipokea kutoka kwa Kristo na kutangazwa na Kanisa. Familia ya Mungu ina kila sababu ya kuwashukuru Mashahidi hawa wa imani, mwaliko kwa waamini kumwachia Kristo ili aweze kuyatawala!

Baba Mtakatifu Francisko akiwa na mawazo ya Kiekumene alisema pia kwamba, Mtume Andrea alikuwa ni ndugu yake Mtakatifu Petro. Andrea ndiye aliyekuwa wa kwanza kadiri ya Maandiko Matakatifu kukutana na Yesu, akamwonesha ndugu yake. Hii ndiyo maana ya uwepo wa ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli ambako Mtume Andrea ni msimamizi wake.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kusali na kumwombea Patriaki Bartolomeo wa kwanza pamoja na Kanisa la Costantinopoli. Ni changamoto ya kuendelea pia kuwakumbuka na kuwaombea Maaskofu wakuu waliovishwa Pallio takatifu, alama ya umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu mwishoni, amewakumbuka na kuwashukuru waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia waliowasindikiza Maaskofu wao wakuu kupokea Pallio takatifu. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amewataka waamini nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ambao kwa sasa wanakabiliana na hali ngumu ya maisha, kusonga mbele kwa imani na matumaini.







All the contents on this site are copyrighted ©.