2013-06-29 14:25:06

Dhamana ya Khalifa wa Mtakatifu Petro ni kuwaimarisha ndugu zake katika imani, upendo na umoja!


Yesu Kristo amempatia Mtakatifu Petro dhamana ya kuwaimarisha ndugu zake katika imani, upendo na umoja. Ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani, iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumamosi tarehe 29 Juni 2013.

Katika Ibada hii ya Misa, Baba Mtakatifu aliwavisha Pallio takatifu, alama ya Kristo mchungaji mwema, Maaskofu wakuu walioteuliwa hivi karibuni, kutoka katika majimbo makuu thelathini na matano.

Ibada ya ya misa takatifu, ilitanguliwa na Maaskofu wakuu kula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na baadaye kuvishwa Pallio takatifu, alama Uaskofu mkuu na baadaye Ibada ya Misa Takatifu ikaendelea kama kawaida. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amewashukuru Maaskofu kutoka sehemu mbali mbali za dunia waliofika mjini Vatican kwa ajili ya kuwasherehekea Miamba wa Kanisa, yaani Watakatifu Petro na Paulo.

Huu ni utajiri mkubwa unaoliwezesha Kanisa kuadhimisha tena na tena lile tukio la Pentekoste ya kwanza, linalounganisha Familia ya Mungu inayozungumza lugha mbali mbali katika imani moja! Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza uliofika mjini Vatican kushiriki katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo, Miamba wa imani. Nyimbo za Ibada ya Misa zimeongozwa na Kwaya ya Kanisa la Mtakatifu Tomasi wa Lipsia; jambo ambalo limepamba Ibada hii na kuonekana kuwa kweli ni ya kiekumene.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Mtakatifu Petro amepewa dhamana ya kuwaimarisha ndugu zake katika mambo makuu matatu. Hii ni dhamana aliyokabidhiwa mara tu baada ya kuungama kwamba, Yesu Kristo alikuwa ni Mwana wa Mungu aliye hai na kwamba, hii ilikuwa ni zawadi ya ufunuo kutoka kwa Baba yake wa mbinguni. Yesu akampatia dhamana na utume unaobubujika kutokana na imani yake kwa Kristo Mwana wa Mungu aliye hai.

Baba Mtakatifu anasema, katika Injili, bado Mitume wa Yesu wameelemewa na mambo ya kidunia, Yesu anapozungumzia kuhusu mateso, kifo na ufufuko wake, hija ambayo Mwenyezi Mungu amemwandalia kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu, Mtume Petro anataka kuweka kizingiti! Anafikiri zaidi kuhusu madaraka, lakini, Yesu anamkanya na kumwambia kwamba, amekuwa ni sehemu ya kikwazo kwake.

Baba Mtakatifu anaonya kwamba, madaraka katika mwono wa kibinadamu ni hatari katika hija ya imani na badala yake, waamini wanapaswa kumwachia Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia zawadi ya imani ambayo ni mwanga wa Kristo katika maisha ya Wakristo na utume ndani ya Kanisa.

Mtakatifu Paulo katika Waraka wake kwa Timotheo anasema kwamba, amevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo ameumaliza, Imani ameilinda! Baba Mtakatifu anasema, Mtakatifu Paulo amevipiga vita si kwa kutumia silaha za zilizotengenezwa kwa mikono ya binadamu ambazo zinaendelea kusababisha maafa makubwa sehemu mbali mbali za dunia, lakini vita aliyopiga ni maisha ya kifodini!

Silaha kubwa aliyokuwa nayo mikononi mwake ni Ujumbe wa Yesu Kristo, zawadi kubwa zaidi katika maisha na utume wake; zawadi ambayo alipenda kuwashirikisha wengine, kiasi kwamba, akajiachilia mikononi mwa Kristo ili aweze kuyamimina maisha yake bila kujihurumia, ili kujenga na kuimarisha Kanisa la Kristo. Askofu wa Roma anachangamotishwa na Mama Kanisa kuwaimarisha ndugu zake katika upendo kwa Kristo, bila ubaguzi wala vikwazo.

Baba Mtakatifu anasema, Askofu wa Roma amepewa dhamana ya kuwaimarisha ndugu zake katika umoja na kwamba, Pallio takatifu walizovishwa Maaskofu wakuu ni kielelezo cha umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro, kielelezo cha umoja na mshikamano katika imani. Uwepo wa umati mkubwa wa Maaskofu kutoka sehemu mbali mbali za dunia ni kielelezo cha umoja unaojionesha katika utofauti. Huu ni Urika wa Maaskofu unaoongozwa na Mtakatifu Petro. Urika huo maadamu umeundwa na wengi, huonesha hali ya Taifa la Mungu ambalo ni la kiulimwengu.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema kwamba, ndani ya Kanisa kuna tofauti kubwa, lakini huu ni utajiri wa Kanisa unaosimikwa katika umoja unaoonesha Mpango wa Mungu, changamoto ya kuvuka vikwazo na kinzani zinazotaka kuligawa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Wote wanapaswa kuungana kwa pamoja, kwani hii ndiyo ile njia iliyoooneshwa na Yesu mwenyewe! Ikiwa kama Pallio ni alama ya umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro, pamoja na Kanisa la Kiulimwengu, basi hii pia ni changamoto ya kila Askofu mkuu kuwa ni chombo cha umoja.

Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni anawaalika waamini kumwachia Mungu mwenyewe nafasi ili aweze kuwafundisha; waweze kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Injili yake, ili kweli waweze kuwa ni wahudumu wa umoja. Hii ndiyo amana kubwa ambayo waamini wameachiwa na Mitume Petro na Paulo; amana inayopaswa kumwilishwa na kila Mkristo. Bikira Maria, Malkia wa Mitume awaombee na kuwasindikiza Maaskofu wakuu katika maisha na utume wao!







All the contents on this site are copyrighted ©.