2013-06-28 08:25:51

Mtakatifu Paulo mwalimu wa mataifa, awe ni mfano wa kuigwa kwa waamini kujishikamanisha na Kristo: kwa mawazo, maneno, lakini zaidi kwa matendo!


Mama Kanisa anapoadhimisha Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani, Askofu mkuu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kwamba, anaguswa kwa namna ya pekee kabisa na maisha na utume wa Mtakatifu Petro mwalimu wa mataifa. RealAudioMP3

Ni mtu aliyepokea imani kwa moyo mkuu na kumfanya Kristo kuwa ni sehemu ya maisha yake. Hisia, fikira, maneno na matendo yalimfanya Mtakatifu Paulo kudiriki hata kusema, kuishi kwake ni Kristo na kwamba, kufa ni faida!

Mtakatifu Paulo alikutana na Yesu Mfufuka kwa njia ya ajabu, hapo akapata wongofu na kuitikia wito wa Kristo, hakajitosa duniani kuufanyia kazi bila ya kujibakiza hata kidogo! Ni kielelezo cha furaha ya Ukristo na changamoto endelevu kwa waamini kujishikamanisha na Kristo, kwa hisia, maneno na matendo yao, kama kielelezo makini cha imani tendaji.

Askofu mkuu Lebulu anasema, maisha ya Mtakatifu Paulo baada ya kuongoka hayakuwa tena na mawaa mbele ya Mwenyezi Mungu. Akaupokea ujumbe wa Habari Njema ya Wokovu, akaumwilisha na kuutangaza hadi miisho ya dunia. Habari Njema ya Wokovu ikawa ni dira na mwongozo wa maisha na vipaumbele vyake, hadi pale alipokatwa kichwa kutokana na imani yake kwa Kristo na Kanisa lake. Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Imani, waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee, kutolea ushuhuda amini wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; kwani Kristo ni Bwana na Mkombozi wa ulimwengu.

Askofu mkuu Josephat Lebulu anawasihi waamini kuimarishwa kwa mifano ya maisha, lakini zaidi kwa mafundisho tanzu yaliyotolewa na Mtakatifu Paulo, ili kuwaonjesha wengine ile furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo!.







All the contents on this site are copyrighted ©.