Maadhimisho ya Mwaka wa Imani: Imani na matumaini ni chanda na pete!
Kanisa Barani Ulaya, "Ecclesia in Europa" ni Waraka wa kichungaji uliotiwa mkwaju
na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili kunako tarehe 28 Juni 2003. Katika Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani, Makatibu wakuu kutoka Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki
Barani Ulaya, kuanzia tarehe 27 Juni hadi tarehe 30 Juni 2013 wanakutana mjini Varsavia,
Poland, ili kupembua kwa kina na mapana athari za myumbo wa uchumi kimataifa, ambao
umetikisa hata misingi ya imani. Kuna baadhi ya watu wanadhani kwamba, kutokana na
maendeleo ya sayansi na teknolojia, imani tena haina nafasi katika maisha na vipaumbele
vyao! Watu wamekata tamaa ya maisha!
Monsinyo Duarte da Cunha, katibu mkuu
wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya anasema kwamba, imani
na matumaini ni chanda na pete na kwamba, Wakristo wanatumwa kutangaza Habari Njema
ya Wokovu hadi miisho ya dunia kwa kuwaonjesha wengine ile furaha na imani inayobubujika
ndani mwao kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Kristo ni kiini cha Uinjilishaji mpya,
dhamana inayofanyiwa kazi na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya
Ukristo.
Athari za myumbo wa uchumi kimataifa ni changamoto kwa waamini kufanya
maamuzi machungu juu ya imani yao: kuendelea kumtumainia Kristo au kujishikamanisha
na masuala ya uchumi na maendeleo ya teknolojia; mambo ambayo bado hayajaweza kuridhisha
ile kiu ya ndani ya mwamini katika hija ya maisha yake hapa duniani? Upendo unaobubujika
kutoka kwa Kristo ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuvunja mipaka
ya ubinafsi, uchoyo na utaifa, ili kuwaonjesha jirani zao ukarimu na upendo. Bado
kuna uwezekano kwa wananchi wa Ulaya kukutana na kuendelea kumtumainia Kristo katika
hija ya maisha yao hapa duniani.
Mkutano wa Makatibu wakuu thelathini na watatu
kutoka Shirikisho la Maabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya, unahudhuriwa na
Padre Raymond O' Toole, Katibu mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki
Barani Asia pamoja na Padre Pietro Felet, Katibu mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya
Maaskofu kutoka katika Nchi Takatifu. Wawakilishi hawa wanashirikisha pia hali ya
Wakristo kutokana katika nchi zao.